Syria yasema itajibu mashambulizi mapya ya Kijeshi yatakayofanywa na Jeshi la Israeli dhidi ya taifa hilo huku Marekani ikijiapiza kuilinda
Imechapishwa: Imehaririwa:
Serikali ya Syria imetishia kujibu mara moja mashambulizi yote mapya ambayo yatafanywa na ndege za kijeshi za Israeli kauli inayokuja baada ya nchi hiyo kutekeleza mashambulizi mawili yaliyolenga kituo cha utafiti wa kijeshi mwishoni mwa juma lililopita. Serikali imeweka bayana haiwezi kuendelea kuvumilia vitendo ambavyo vitakuwa vinafanywa na majeshi ya Israeli katika ardhi ya Damascus ambavyo vinakwenda kinyume na serikali za mipaka ya kimataifa.
Marekani imeeleza licha ya kuwepo kwa vitisho hivyo vya Syria kuelekezwa kwa Israeli lakini Marekani imesema itaendelea kuhakikisha inamlinda rafiki yake mkubwa Israeli asikabiliwe na mashambulizi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel amesisitiza hawatokuwa tayari kuona rafiki zao hao wakubwa wakishambuliwa kwa namna yoyote ile na watahakikisha Taifa hilo linakuwa salama.
Damascus pia imepokea kwa mikono miwili makubaliano yaliyofikiwa baina ya Marekani na urusi katika kuhakikisha umwagaji wa damu unakoma mara moja katika nchi hiyo baada ya kudumu kwa kipindi cha miezi 26 na kuchangia vifo vya maelfu ya raia.
Licha ya Serikali ya Damascus kupongeza hatua ya Marekani na Urusi kuwa tayari kusimamia upatikanaji wa amani ya kudumu nchini Syria lakini wamepinga mkakati wa kujiuzulu kwa Rais Bashar Al Assad.
Tayari Marekani kupitia Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry amesema msimamo wao ni kuhakikisha Rais Assad anakaa kando na ndipo iundwe serikali ya mpito itakayohusika kwenye suluhu ya kisiasa.
Waziri Kerry amesema kile kinachopaswa kufanyika kwa sasa ili kupata suluhu ya umwagaji wa damu nchini Syria ni kuanza upya kwa mazungumzo ambayo hayapaswi kumshirikisha Rais Assad.
Haya yanakuja kipindi hiki ambacho Kundi la Hezbollah lenye maskani yake nchini Lebanon likitangaza kuwa na wapiganaji wake nchini Syria ambao wanashirikiana na serikali kwenye vita vinavyoendelea.
Kiongozi wa Kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah ndiye amethibitisha uwepo wa wapiganaji wake nchini Syria huku akikiri vita hivyo kwa sasa vimechukua sura mpya kabisa kutokana na mataifa mengine kuingilia.
Nasrallah amekiri kumekuwa na matumizi makubwa ya silaha hatari ambazo zinatumika kwenye vita hivyo vya kutaka kuing'oa serikali ya Rais Assad iliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Kiongozi huyo wa Hezbollah amepongeza hatua ya serikali ya Damascus kutojibu mashambulizi yaliyofanywa na Jeshi la Israeli na kuonesha Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.