TANZANIA-DRC

Wanajeshi wa Tanzania wawasili DRCongo kukabiliana na waasi

Kundi la kwanza la wanajeshi 100 toka nchini Tanzania limewasili jumamosi hii katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC katika mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa UN wa kukabiliana na makundi ya waasi, Umoja wa Mataifa UN umearifu. Tanzania inatarajia kupeleka jumla ya wanajeshi wake 1280 katika mpango huo.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo ni utekelezaji wa azimio la Machi 28 lililopitishwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa UNSC wa kuunda brigedi maalumu ya kupambana na waasi katika eneo la mashariki mwa DRCongo.

Msemaji wa mpango huo Felix Basse amesema Tanzania imekuwa ni nchi ya kwanza kupeleka wanajeshi wake katika eneo hilo, wanajeshi zaidi toka Malawi na Afrika Kusini wanaarajiwa kujiunga na kikosi hicho wakati wowote kuanzia hivi sasa.

Wanajeshi zaidi ya 3000 watadhibiti makundi ya waasi zaidi ya 25 katika mkoa wa Kivu pekee, tayari kundi la waasi la M23 limeripotiwa kujiandaa ili kujibu mashambulizi yatakayoelekezwa kwako na vikosi hivyo vya UN.

Jeshi la DRCongo kwa muda mrefu limeshindwa kutokomeza makundi la waasi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo, hata hivyo mamlaka za nchi hiyo zinatarajia mpango wa sasa wa UN huenda ukazaa matunda mema katika usalama wa nchi hiyo.