DRC

Waasi 15 wa M23 na wanajeshi wanne wa serikali ya DRC wauwawa kufuatia mapigano mapya Kaskazini mwa Goma

Wanajeshi wa serikali ya DRC
Wanajeshi wa serikali ya DRC Presstv.ir

Waasi 15 wa M23 na wanajeshi wanne wa serikali ya DRC FARDC wameuwawa kufuatia mapigano mapya yaliyoibuka tena leo Jumanne huko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  vyanzo vya kijeshi vimesema, siku moja kabla katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kutembelea eneo hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Kanali Olivier Hamuli, msemaji wa jeshi la Kongo (FARDC) katika jimbo la Kivu Kaskazini, amesema kuwa vikosi vya M23 vimeshambuliwa maeneo ya jeshi la serikali ya Congo FARDC katika eneo hilo hilo vililoshambulia jana Jumatatu, wakati mapigano yalipozuka kilomita 12 Kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa mkoa .

Hamuli ameongeza kuwa wanafanya mashambulizi ambayo ni ya kwanza kushirikisha askari waasi wa M23 tangu mwezi Desemba.

Katibu Mkuu Ban Ki-moon atatembelea nchini DRC kesho jumatano katika ziara ambayo itamfikisha Goma pamoja na nchi jirani ya Rwanda na Uganda, ambayo serikali ya Congo na Umoja wa Mataifa inazituhumu kuwafadhili waasi wa M23 huku nchini zote mbili zikikanusha tuhuma hizo.

Mtaalamu wa kijeshi kutoka mataifa ya Magharibi amesema kuwa waasi wa M23 wanapambana kwa vinu na magari ya kivita yaliyotekwa kutoka majeshi ya serikali mwezi Novemba mwaka jana. Huku jeshi la serikali FARDC likitumia mizinga.