DR Congo-Umoja wa mataifa UN

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa UN Ban Ki Moon ahimiza operesheni za kijeshi kuharakishwa mashariki ya DRC.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon asisitiza operesheni dhidi ya uasi kuanza haraka mashariki ya jamuhuri ya demokrasia ya Congo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon asisitiza operesheni dhidi ya uasi kuanza haraka mashariki ya jamuhuri ya demokrasia ya Congo. AFP

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon amesisitiza kuharakishwa kwa operesheni ya kijeshi ya vikosi maalumu vya Umoja wa mataifa kukabiliana na uasi mashariki mwa jamuhuri ya demokrasia ya Congo,uasi ambao umeanza kushuhudiwa juma hili ukukithiri wakati huu akiwasili mjini Kinshasa tayari kuzuru eneo la mashariki.

Matangazo ya kibiashara

Katibu mkuu Ban amesema kuwa kulingana na hali iliyojitokeza juma hili kwa waasi kushambulia makazi ya watu na wanajeshi wa serikali, hakuna budi zaidi ya kuharakisha kusambazwa kwa wanajeshi wa UN kukabiliana na wapiganaji hao kikamilifu.

Kwa upande wa serikali ya DRC, imesema kuwa inashangazwa na waasi wa M23 kutaka kung'ang'aniza kukutana na katibu mkuu licha ya yeye mwenyewe kuwataka kwanza kuweka silaha chini ndipo wafanye mazungumzo.

Nao wabunge wa bunge la kitaifa wamekosoa kauli ya baadhi ya wabunge wa upinzani ambao wanataka kukutana peke yao na katibu mkuu na kuongeza kuwa wanashangazwa na hatua hiyo kwakuwa sasa walipaswa kuonesha umoja.

Katibu mkuu Ban Ki Moon anaanza ziara rasmi nchini DRC ambapo atakuwa na mazungumzo na rais Joseph Kabila mjini Kinshasa kabla ya kuelekea mashariki mwa nchi hiyo kushuhudia hali ilivyo.

Katika hatua nyingine naye Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi za ukanda wa maziwa makuu, Mary Robinson ameendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano yaliyoibuka juma hili kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa serikali mashariki mwa nchi hiyo kwenye mji wa Goma.

Bi Robinson amesema kuwa wanaoathirika ni wananchi na sio wanajeshi wanaopigana huku akisikitishwa na kuendelea kushuhudiwa kwa machafuko mashariki mwa nchi hiyo licha ya wakati wa ziara yake kuzitaka pande hizo mbili kuheshimu mkataba wa kimataifa wa amani kuhusu DRC.