SYRIA-URUSI-UINGEREZA

Uingereza yasisitiza suluhu ya mzozo Syria ni Assad kuondoka madarakani

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza,William Hague
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza,William Hague REUTERS

 Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague amesema kuwa suluhu pekee ya mzozo wa syria ni raisi Assad kujiondoa madarakani.Kiongozi huyo amesema hayo wakati huu kuelekea mjadala wa kimataifa unaohusu jitihada za kuleta amani ya Syria.

Matangazo ya kibiashara

Hague amesisitiza mbele ya waandishi wa habari kuwa ni msimamo wa Uingereza kwa muda mrefu kuwa hakuna suluhu ya mzozo wa Syria ikiwa Assad atasalia madarakani.

Nchi marafiki za Syria zinataraji kukutana na Upinzani huko Amman kujadili pendekezo la Marekani na Urusi juu ya mkutano wa amani ambao Hague amesisitiza kuwa ni makubaliano ya serikali ya mpito kuwa na mamlaka kamili.

Mapema jumatano Upinzani nchini Syria umetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa na jukwaa la kushughulikia misaada ya kibinadamu kwa lengo la kusaidia mji wa Qusayr ambapo kumeshuhudia mapigano makali kati ya majeshi ya serikali ya Syria dhidi ya waasi.

Kaimu mkuu wa muungano wa taifa George Sabra ametoa wito huo kwa jumuiya ya kimataifa kwa kuitaka kufungulia misaada ya kibinadamu kuwaokoa majeruhi,kuwapelekea madawa na usaidizi takribani watu elfu hamsini.

Wakati huohuo taarifa zinaeleza kuwa naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Faisal Muqdad anatarajia kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov jumatano mjini Moscow katika mkutano uliolenga kumaliza machafuko nchini Syria.

Duru za habari nchini humo zimebainisha kuwa Muqdad na Lavrov watajadiliana juu ya maandalizi ya mkutano wa amani ambao ni makubaliano ya wanadiplomasia wa Urusi na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alipokuwa katika ziara yake nchini humo mapema mwezi huu.

Urusi imeendelea kuonekana kuwa mshirika wa muhimu wa utawala wa raisi wa Syria Bashar Al Assad huku mataifa ya magharibi wakiitaka serikali ya Moscow kuitumia fursa yake kuisaidia kukomesha mgogoro wa Syria ambao umedumu kwa takribani miaka miwili sasa baina ya serikali dhidi ya waasi.