Tanzania

Watu 90 washikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika kwenye vurugu Mtwara Tanzania

Raisi wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete
Raisi wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete AFP

Jeshi la polisi nchini Tanzania linawashikilia zaidi ya watu 90 waliohusika katika vurugu za maandamano ya kupinga kusafirishwa kwa gesi mkoani Mtwara jumatano na kusababisha kifo cha mtu mmoja,Waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania Emmanuel Nchimbi amethibitisha ambapo kwa sasa hali ya utulivu imerejea na kubainisha makazi kadhaa na mali vimeharibiwa kufuatia purukushani za waandamanaji.

Matangazo ya kibiashara

Akiwa ziarani mkoni Dodoma rais wa Tanzania, Daktari Jakaya Mrisho Kikwete amekemea vurugu zilizotokea jumatano na kutaka polisi kufanya kazi yao na kuahidi serikali yake kutovumilia vitendo kama hivyo kamwe.

Raisi Kikwete amesema rasilimali zilizopatikana Mtwara zitatumika kwa ajili ya manufaa ya wote pamoja na maeneo ambayo rasilimali zinatoka,hivyo kuwataka wakazi wa Mtwara kutodhani wamesahaulika kwani mipango kabambe ya kutumia gesi kujenga viwanda mbalimbali vitakavyoleta maendeleo Mtwara.

Hali ya usalama imeelezwa kurejea kwenye maeneo mengi mkoani Mtwara ambapo rfikiswahili imemtafuta kamanda wa polisi wa Mkoa, Linus Simnzumwa ambaye naye alithibitisha hali ya usalama kudhibitiwa.

Hii ni mara ya pili kwa waandamanaji mkoani mtwara kuchoma moto mali za serikali wakipinga ujenzi wa bomba la gesi, huku serikali kupitia kwa waziri wa nishati na madini Sospeter Muhongo ikisisitiza kuendelea na ujenzi huo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake.

Wakati wa kikao cha jioni cha bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, spika wa bunge Anna Makinda alilazimika kuahirisha kikao hicho na kuiagiza serikali kutoa maelezo kwenye kikao cha alhamisi.