Ripoti ya tume ya ukweli haki na maridhiano yapendekeza raisi Uhuru kuomba radhi
Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu ripoti iliyotolewa na tume ya maridhiano nchini Kenya ambayo imemtaka rais Uhuru Kenyatta pamoja na viongozi wengine kuomba radhi kutokana na machafuko ya mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Imechapishwa:
Ripoti hiyo imemtaja rais Kenyatta na naibu wake William Ruto kuhusika na vurugu za mara baada ya uchaguzi huku mwenyekiti aliyewasilisha ripoti hiyo balozi Bethuel Kiplagat nae akitajwa kuhusika mauaji ya halaiki ya Wagalla mwaka 1984.
Lakini balozi Kiplagat anaona kuwa suala la raisi Uhuru kuomba msamaha ni sawa pia ni vema kuwapa pole raia wote walioathiriwa na matukio ya ukatili dhidi ya haki za binadamu ingawa haitaweza kusaidia wote.
Aidha amesema yuko tayari kufanyiwa uchunguzi zaidi kwa tuhuma za kuhusika na kutoa agizo la mauji ya Wagala miaka ya themanini Kaskazini mwa Kenya na pia kunyakua ardhi ya umma alipokuwa anahudumu serikalini.
Raisi wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wametajwa kuhusika katika vurugu za baada za uchaguzi katika ripoti iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na gamu kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Kenya kuanzia Uhuru wa taifa hilo 1963.
Kwa niaba ya watu walioathirika na matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu tume ya ukweli na maridhiano imependekeza viongozi hao kuomba radhi kwa Wakenya.
Hata hivyo madai hayo ya tume yamepingwa na raisi Kenyatta na naibu wake.
Tume ya ukweli haki na maridhiano iliundwa kufuatia machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu miaka mitano iliyopita kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Kenya.