NIGERIA-MAREKANI

Marekani yaitaka Nigeria kutokiuka haki za binadamu katika oparesheni yake dhidi ya Boko Haram

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameionya Nigeria kuhakikisha jeshi lake halihusiki na unyanyasaji dhidi ya raia wakati inapoendelea na oparesheni yake ya kutokomeza wapiganaji wa kiislamu nchini humo.

REUTERS/Akintunde Akinleye
Matangazo ya kibiashara

Kerry ambaye amekuwa na mazungumzo mafupi na Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan mjini Addis Ababa Ethiopia wakati wa sherehe za miaka hamsini ya Umoja wa Afrika AU amesisitiza mamlaka za Nigeria hazipaswi kuendesha oparesheni kwa kulipiza kisasi kwa raia ambao wengi wao hawana hatia.

Pembezoni mwa sherehe hizo, Kerry aliwaambia wanahabari kuwa Nigeria ina haki ya kujilinda dhidi ya Boko Haram lakini inapaswa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.

Hivi karibuni Rais Jonathan alilazimika kutangaza hali ya hatari katika majimbo matatu kutokana na Boko Haram kuzidi kutekeleza huku jeshi la nchi hiyo likijiapiza kuhakikisha wanawasaka wanamgambo na magaidi wanaofanya mauaji.

Boko Haram wanatuhumiwa kusababisha mauaji ya watu takribani 3600 wakiwamo wanausalama tangu lilipoanzisha harakati zake mwaka 2009 wakipinga utolewaji wa elimu ya Magharibi.