AFRIKA

Viongozi wa nchi wanachama wa AU kujadili changamoto zinazolikabili bara la Afrika

www.thelondoneveningpost.com

Maadhimisho ya miaka hamsini ya Umoja wa Afrika AU yameendelea mjini Addis Ababa Ethiopia ambapo viongozi toka nchi wanachama wanashiriki katika mkutano wa umoja huo unaojadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Afrika. Akifungua sherehe hizo siku ya jumamosi Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn aliwataka viongozi wa Afrika kuimarisha umoja huo kwa kupiga vita umasikini na migogoro inayoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya nchi wanachama.

Matangazo ya kibiashara

Kwa upande wake Mwenyekiti wa AU Nkosazana Dlamini-Zuma amesisitiza kuwa migogoro inayolikabili bara hili itakomeshwa kwa mshikamano na umoja utakaoonyeshwa na wahusika.

Viongozi mashuhuri waliohudhuria sherehe hizo toka nje ya bara hili ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki-moon, Rais wa Ufaransa Francois Hollande, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, Naibu wa Waziri Mkuu wa China Wang Yang na Rais wa Brazili Dilma Rousseff.

Sherehe hizo pia zilishuhudia serikali ya Brazili ikiweka wazi mpango wa kutajka kusamehe madeni ya jumla ya dola za Marekani milioni mia tisa katika nchi kumi na mbili za Afrika, miongoni mwa nchi zitakazonufaika na msamaha ni Tanzania, Congo-Brazzaville na Zambia.

Viongozi toka nchi wanachama hamsini na nne wanashiriki mkutano ulioambatana na sherehe hizo ambapo kwa pamoja wataangazia pendekezo la Mawaziri wa mambo ya nje wa AU kuitaka mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC kurejesha nchini Kenya kesi ya washukiwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 inayomkabili Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Rutto pamoja na Mtangazaji wa Redio Joshua Arap Sang.

Ajenda nyingine zinazopewa kipaumbele ni hali ya kisiasa nchini Mali na oparesheni za kutokomeza makundi ya kigaidi, mpasuko wa kisiasa katika visiwa vya Madagascar halikadhalika juhudi za kusaka amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa UN.