PARIS-UFARANSA

293 wakamatwa kufuatia maandamano ya kupinga ndoa za jinsia moja jijini Paris, Ufaransa

Polisi jijini Paris, Ufaransa wamekabiliana na maelfu ya waandamanaji wanaopinga sheria iliyoidhinishwa na bunge kuruhusu ndoa za watu wa jinsia moja.  

Waandamanaji wakipambana na polisi jana jioni mjini Paris, Ufaransa
Waandamanaji wakipambana na polisi jana jioni mjini Paris, Ufaransa Reuters
Matangazo ya kibiashara

Maandamano hayo ambayo awali yalianza kwa amani yaligeuka kuwa vurugu pale ambapo polisi walilazimika kuingilia kati kuwatawanya waandamanaji hao ambao walianza kuharibu mali.

Waandishi kadhaa wa habari walishambuliwa na waandamanaji hao, hali iliyowalazimu polisi kuingilia kati kuwanusuru kutokana na kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira baada ya kuwatuhumu kuunga mkono ndoa hizo.

Polisi jijini Paris wanasema kuwa inawashikilia watu zaidi ya 293 ambapo watu sita ndio wanaoelezwa kujeruhiwa kutokana na maandamano hayo wakiwemo polisi wanne waliokuwa wakishiriki kwenye operesheni hiyo.

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Manuel Valls amelaani maandamano hayo yaligeuka kuwa vurugu, na kuyashutumu makundi yenye msimamo mkali kuhusu ndoa za jinsia moja nchini humo.

Maandamano hayo yamefanyika wakati huu ambapo jopo la majaji wa tamasha la filamu la Cannes wakitoa tuzo ya filamu bora ya mwaka kwa mtunzi mwenye asili ya Tunisia na Ufaransa aliyetengeneza filamu inayoitwa :Blues is the Warmest Colour" ambayo inaelezea maisha ya wanawake waliooana.

Waandaji wa maandamano hayo wanasema kuwa zaidi ya watu milioni moja walijitokeza kwenye maandamano hayo kuoinga sheria hiyo inayoruhusu ndoa za watu wa jinsia moja.