UINGEREZA-KENYA

Adebolajo aliwahi kukamatwa nchini Kenya, Uingereza yaunda kikosi maalumu kupambana na makundi yenye msimamo

Serikali ya Kenya jana jioni imedhibitisha kuwa mmoja wa watuhumiwa waliohusika na mauaji ya mwanajeshi mmoja wa Uingereza mjini London, alishawahi kushikiliwa nchini humo mwaka 2010 akihusishwa kuwa na uhusiano na wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia.

Michael Adebolajo wa tano kutoka kushoto akionekana na watuhumiwa wengine mwaka 2010 wakati alipokamatwa na maofisa wa Kenya
Michael Adebolajo wa tano kutoka kushoto akionekana na watuhumiwa wengine mwaka 2010 wakati alipokamatwa na maofisa wa Kenya Reuters
Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Serikali ya Kenya, Muthui Kariuki amedhibitisha mtuhumiwa huyo kuwahi kushikiliwa nchini Kenya na baadae kuachiliwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha dhidi yake.

Kariuki ameongeza kuwa baada ya kukosekana kwa ushahidi waliamua kumkabidhi kwa maofisa usalama wa Uingereza MI5 ambao walimchukua hadi nchini Uingereza kwa mahojiano.

Hata hivyo Serikali ya Kenya kupitia msemaji wake imekanusha taarifa kuwa mtuhumiwa Michael Adebolajo wakati akishikiliwa na maofisa wa Kenya alinyanyaswa akiwa gerezani hali iliyomfanya abadili mwennedo wake.

Wakati akikamatwa mwaka 2010 Adebolajo alikuwa akituhumia jina jingine tofauti na lile ambalo sasa limebainika nchini Uingereza.

Serikali ya Uingereza imekosolewa kutokana na kushindwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mtuhumiwa huyo na kwamba kitendo cha maofisa wa MI5 kutaka kumtumia kuchunguza makundi ya waislamu wenye msimamo mkali nchini humo kulichochea kutekeleza mauaji hayo.

Shemeji wa Adebolajo anasema kuwa mara kadhaa maofisa wa MI5 walimhoji na kumshinikiza akubali kushirikiana nao kupeleleza makundi mengine ya waislamu nchini humo hatua aliyokataa na kisha kuanza kutoa upinzani kwa MI5.

Kufuatia mauaji hao, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ametangaza Serikali yake kuunda kikosi maalumu cha kupambana makundi yenye msimamo mkali nchini Uingereza.

Wabunge wameongeza shinikizo zaidi kwa Serikali ya waziri mkuu Cameron kutoa maelezo ya kina kuhusu mtuhumiwa Michael Adebolajo na mwenzake kabla ya kutekeleza mauaji.

Polisi nchini Uingereza wanaendelea na msako wa watuhumiwa wengine ambao wanadaiwa kuwa na uhusiano na mtuhumiwa huyo ambapo hapo jana watu wanne zaidi walikamatwa na kuachiwa kwa dhamana hii leo.