MADAGASCAR

Chisano: Hakutakuwa na suluhu iwapo Andry Rajoelina atawania urais

Mpatanishi wa mzozo wa kisiasa nchini Madagascar, rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chisano ameendelea na juhudi zake za kujaribu kumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo licha ya upinzani anaokabiliana nao.

Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina
Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina Reuters
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumamosi rais wa Madagascar, Andry Rajoelina alitoa masharti kwa mpatanishi huyo akidai kuwa ataondoa jina lake kwenye kinyang'anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao iwapo wapinzani wake nao watafanya hivyo.

Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC ndio unasimamia mazungumzo ya kutafuta suluhu nchini Madagascar ambao wamekuwa wakimshawishi Rajoelina na Marc Ravalomanana kuweka tofauti zao pembeni na kushiriki mazungumzo ya kuleta suluhu nchini humo.

Mpatanishi wa mzozo huo, Joachim Chisano, amesema kuwa anasikitishwa na hali inayoendelea nchini Madagascar na kwamba kuendelea kung'ang'ania kusalia madarakani kwa baadhi ya viongozi kutachelewesha kupatikana kwa amani nchini humo.

Baadhi ya viongozi wanaopingwa na rais Rajoelina ni pamoja na mke wa rais wa zamani wa nchi hiyo Marc Ravalomanana ambaye amepitishwa na tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo kuwania urais.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa iwapo rais Rajoelina atawania nafasi ya urais kutaendelea kuweka msingi mgumu wa kupatikana kwa suluhu ya kisiasa nchini humo.

Nchi ya Madagascar imekuwa kwenye mzozo wa kisiasa toka kuingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi kwa rais Rajoelina akiupindua utawala wa Marc Ravalomanana.

Rajoelina na Ravalomanana wote walitangaza kutowania nafasi ya urais kwenye uchaguzi wa Mwezi July mwaka huu, lakini katika hatua ya kushangaza, rasi Rajoelina aliwasilisha jina lake kwa tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo.