UMOJA WA AFRIKA-AU

Viongozi wa AU kumaliza mkutano wa siku mbili hii leo, maazimio kuhusu DRC na ICC kutolewa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wakati akihutubia mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta wakati akihutubia mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU Reuters

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU, unafikia kilele hii leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, huku mjadala kuhusu mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na suala la mahakama ya ICC ukichukua nafasi.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 toka kuanzisha kwa Umoja huo kutoka nchi huru za Afrika OAU na baadae kuundwa kwa Umoja wa Afrika baada ya mataifa mengi kupata uhuru wake.

Suala la mzozo wa mashariki mwa DRC limechukua nafasi kwenye mazungumzo haya ya siku mbili ambapo marais wanajadiliana namna ya kuhakikisha amani inarejea mashariki mwa DRC wakati huu viokosi vya Tanzania, Malawi na Afrika Kusini vikitarajiwa kuanza opereasheni ya kukabiliana na waasi wa M23.

Mkutano huu kwa mara ya kwanza umewakutanisha marais toka nchi za ukanda wa maziwa makuu toka kusaini makubaliano ya kusaka amani mashariki mwa DRC kwa kuidhinisha kikosi maalumu kitakachokabiliana na makundi ya waasi nchini humo.

Pembezoni mwa mkutano huo, rais wa Tanzania, Daktari Jakaya Mrisho Kikwete amesema mazungumzo yao yamepiga hatua na kwamba kuungwa mkono kwa hatua ambazo nchi za ukanda wao zilifikia kuhusu mzozo wa DRC ni ishara tosha ya ushindi dhidi ya makundi ya uasi mashariki mwa DRC.

Tanzania inatuma zaidi ya wanajeshi elfu moja na mia mbili themanini (1280) kuungana na wanajeshi wengine wa Umoja wa Mataifa ambao watakakuwa na mamlaka ya kukabiliana na makundi ya waasi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon amesita kwa mara nyingine kuweka wazi hasa ni lini operesheni hiyo itaanza lakini akasisitiza kuwa ni lazima kuwe na mpango wa amani ambao utawashawishi waasi kuweka silaha chini kabla ya kukabiliana na vikosi vyao.

Mbali na mzozo wa DRC, viongozi hao pia wamejadili mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali ya Kenya kuitaka mahakama ya kimataifa ya ICC kufuta kesi dhidi ya viongozi wa Kenya rais Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto ambao wanashtakiwa kwa makosa ya kuchochea vurugu na kushiriki vitendo vya ukiukaji haki za binadamu mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Mapendekezo hayo ambayo yalikubaliwa kwa kauli moja na mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo, yanataka mahakama ya ICC irejeshe kesi hizo kwenye mahakama za Kenya.

Hata kama viongozi hao watakubaliana na mapendekezo ya Kenya, uamuzi wao hautaathiri mwenendo wa kesi ambayo inaendelea kwenye mahakama ya ICC.

Mapendekezo hayo yaliungwa mkono na rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir ambaye amewataka viongozi wa Umoja huo kuungana kupinga kesi zinazohusu viongozi wa Afrika kupelekwa kwenye mahakama hiyo.

Mwishoni mwa mkutano huu, viongozi hawa watatoka na maazimio ya mambo ambayo watakubaliana kuhusu mzozo wa DRC na suala la mahakama ya ICC.