UGANDA-UINGEREZA

Wakili wa Jenerali David Sejusa, asema mteja wake hana mpango wa kurejea nchini Uganda hivi karibuni

Jenerali wa jeshi la Uganda ambaye hivi karibuni alivujisha siri za kutakiwa kuuawa kwa maofisa kadhaa wa jeshi kutokana na msimamo wao wa kupinga mpango wa kurithishwa madaraka kwa mtoto wa rais Museveni, ameomba ulinzi toka kwa polisi wa Uingereza. 

Aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa nchini Uganda, Jenerali, David Sejusa ambaye sasa anaomba ulinzi wa polisi wa Uingereza
Aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa nchini Uganda, Jenerali, David Sejusa ambaye sasa anaomba ulinzi wa polisi wa Uingereza Reuters
Matangazo ya kibiashara

Jenerali, David Sejusa ambaye alikuwa ni mkuu wa usalama wa taifa nchini humo hatarajii kurejea nchini mwake hivi karibuni kutokana na kitisho cha usalama wake iwapo atafanya hivyo, wakili wake Joseph Luzige amedhibitisha.

Luzige amesema kuwa mteja wake amekuwa chini ya Uangalizi maalumu toka awasili nchini Uingereza kutokana na kuwepo taarifa kuwa kuna maofisa usalama wa Uganda ambao wako nchini humo kwa lengo la kumuua.

Wakili huyo ameongeza kuwa mteja wake ameomba ulinzi wa polisi wa Uingereza na kwamba anahofia maisha yake kutokana na barua aliyoitoa hivi karibuni na kuchapishwa kwenye gazeti la Daily Monitor.

Kwenye barua hiyo, Jenerali, Sejusa ameeleza mpango wa Serikali wa kutaka kuwaua baadhi ya maofisa wa jeshi na wale wa Serikali ambao wanapinga mpango wa rais Museveni kumuandaa mtoto wake kurithi madaraka.

Jenerali Sejusa alikuwa kiongozi mkuu wa maofisa usalama nchini Uganda na wale wa kimataifa ambapo amekuwa akitoa maagizo ya kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya viongozi mbalimbali kabla ya kuhamishiwa kwenye wizara ya mambo ya ndani ya nchi.

Kwenye barua yake iliyovujishwa kwa vyombo vya habari, jenerali Sejusa, amemtaja Brigedia Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto mkubwa wa rais Museveni kuandaliwa na baba yake kurithi madaraka yake kutokana na kupandishwa vyeo kwa haraka na kuwa kiongozi wa taasisi muhimu za kiusalama ukiwemo ulinzi wa baba yake.

Msemaji wa jeshi la Polisi nchini Uganda, Judith Nabakooba amekataa kusema chochote kuhusiana na tukio hilo na kwamba hajapewa maelekezo yoyote toka kwa viongozi wake wa juu.

Juma moja lililopita polisi nchini Uganda walivamia ofisi za gazeti la Daily Monitor na magazeti mengine pamoja na vituo vya redio wakilenga kutafuta barua hiyo ambayo hata hivyo bado haijafanikiwa kuipata.