AU-ICC

Mahakama ya ICC yapuuza madai ya viongozi wa Umoja wa Afrika kuhusu kuwalenga viongozi wa bara hili pekee

Le président kényan Uhuru Kenyatta.
Le président kényan Uhuru Kenyatta. Reuters

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC imetupilia mbali madai yaliyotolewa na viongozi wa Umoja wa Afrika AU kuwa mahakama hiyo ni yakibaguzi na inalenga viongozi wa bara hilo.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa mahakama hiyo, Fadi El Abdallah amesema kuwa mahakama ya ICC haikubaliani na kauli zilizotolewa na viongozi wa Umoja wa Afrika na kwamba kamwe mahakama hiyo haina mpango wa kurejesha kesi inayomkabili rais wa Kenya na naibu wake nchini humo.

Mahakama hiyo imesisitiza kuwa, kesi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta na naibu wake zitaendelea kusikilizwa kwenye mahakama hiyo kama ilivyopangwa na kwamba hakuna uwezekano wala kufikiria ombi la viongozi hao kutaka kesi zao zisilizwe kwenye mahakama za ndani.

Kauli ya mahakama ya ICC inatolewa punde baada ya viongozi wa Umoja wa Afrika kumaliza mkutano wao mjini Addis Ababa, Ethiopia na kutoa kauli nzito dhidi ya mahakama hiyo, ya kwamba ni yakibaguzi na inalenga viongozi wa Afrika peke yake.

Mkutano wa siku mbili wa viongozi wa Afrika ulitawaliwa na ajenda kuhusu mahakama ya ICC ambapo nchi ya Uganda ndio iliyowasilisha pendekezo la kujadiliwa kwa suala hilo na kutaka kesi dhidi ya rais wa Kenya na naibu wake zirejeshwe nchini mwao.

Mahakama ya ICC mjini The Hague ambayo ilibuniwa mwaka 2002 kwa lengo la kushughulikia kesi za wahalifu wa kivita, imekuwa ikikosolewa vikali na viongozi wa Afrika kwa madai kuwa inawalenga zaidi viongozi wa bara hilo.

Hivi karibuni mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda aliwaambia majaji wanaosikiliza kesi dhidi ya viongozi wa Kenya, kuwa nchi hiyo imeendelea kukaidi kushirikiana na ofisi yake kuhusu kuwapataia baadhi ya nyaraka muhimu kwenye mwenendo wa kesi yao.

Ikumbukwe ya kuwa nchi nyingi za Afrika ambazo zimesaini mkataba wa kuitambua mahakama hiyo zilitia saini kwa hiari yao jambo ambalo linawabana pindi wanapotaka kujitoa kwenye mahakama hiyo.