KAMPALA-UGANDA

Polisi: Hakuna ofisi itakayofunguliwa mpaka watoe barua tunayoisaka

Polisi nchini Uganda imeendelea kusisitiza kuwa vituo vya habari vilivyofungwa kutokana na kukataa kutoa barua ambazo inazitafuta vitaendelea kufungwa mpaka pale viongozi wake watakapokubali kushirikiana nao.

Moja ya ofisi za vyombo vya habari vilivyofungwa mjini Kampala zikilindwa na polisi
Moja ya ofisi za vyombo vya habari vilivyofungwa mjini Kampala zikilindwa na polisi Reuters
Matangazo ya kibiashara

Vituo vinne vya habari vilitangazwa kufungwa na polisi juma moja lililopita baada ya wahariri wake kukataa kuonesha barua zinazosakwa na polisi na kudaiwa kutolewa na aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa David Sejusa.

Mwandishi wetu wa Kampala Tonny Singoro amesema kuwa ofisi za gazeti la Daily Monitor zimeendelea kufungwa na kuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kwamba havitegemewi kufunguliwa hivi karibuni.

Akizungumza mjini Kampala, kamanda wa Polisi, Kale Kayihura amesisitiza jeshi lake kuendelea kuzifunga ofisi hizo mpaka pale wahariri wake watakapotoa barua ambazo wanazitafuta na zilichapishwa kwenye vyombo hivyo vya habari.

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Uganda wameendelea kukosoa hatua hiyo ya Serikali wakidai inakwenda kinyume na haki za binadamu kwakuwa inawanyima haki wananchi kupata habari.

Barua iliyotolewa na jenerali David Sejusa ilieleza mpango wa Serikali ya rais Museveni kuhusu kumuandaa mtoto wake kumrithi madaraka pindi atakapotangaza kuondoka madarakani.