SUDAN-SUDAN KUSINI

Rais wa Sudan atishia kulifunga bomba la mafuta linalotoka Sudan Kusini

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ametishia nchi yake kulifunga kabisa bomba lake la mafuta linalotoka nchini Sudan Kusini kuelekea kwenye pwani ya bahari ya Khartoum iwapo nchi hiyo haitaacha kuwaunga mkono waasi wa Sudan.

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir Reuters
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kupitia njia ya Televisheni, rais Bashir amesema kuwa Serikali yake italifunga bomba hilo la mafuta iwapo serikali ya Juba itaendelea kuwaunga mkono waasi wanaopigana kwenye jimbo la Darfur wakilenga kumpindua.

Rais Bashir amesema kuwa hili ni onyo lake la mwisho kwa Serikali ya Juba na kwamba italifunga kabisa bomba hilo iwapo Juba itaendelea kushirikiana na waasi wa Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile ambao wamekuwa wakipigana na Serikali.

Kundi la waasi wa SRF wameanzisha mashambulizi mapya kwenye baadhi ya maeneo nchini Sudan na sasa wanaumiliki mji wa Um Rawaba ulioko katikati mwa nchi hiyo.

Hivi karibuni pia kundi la SPLM-North lilitangaza kujiunga na waasi wa Darfur, JEM na wale waliojitenga kutoka jeshi la Sudan SLA ambao waliunda kundi la Sudan Revolutionary Front SRF mwishoni mwa mwaka jana.

Toka nchi ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan kati kati ya mwaka 2011 nchi hizo zimekuwa zikivutana kuhusu uzalishaji wa mafuta na kugombea mpaka jambo ambalo mara kadhaa lilisababisha nchi hizo kutumbukia kwenye vita.

Serikali ya Juba imekanusha kushirikiana na makundi ya waasi wa Darfur wanaopigana nchini Sudan na kwamba yenyewe inapambana na waasi ambao wanaendesha mashambulizi kwenye jimbo la Jonglei.