SUDAN-SUDAN KUSINI

Juba: Tutaheshimu mkataba wa amani na hatuna uhusiano na makundi ya waasi wa Darfur

Serikali ya Sudan Kusini imesema itaendelea kuheshimu mkataba wa amani waliotia saini kati yake na Sudan siku moja baada ya rais wa Sudan, Omar al-Bashir kutishia kulifunga bomba kuu la kusafirisha mafuta kutoka Sudan Kusini.

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir akiwa na mwenzake wa Sudan Kusini, Salva Kiir
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir akiwa na mwenzake wa Sudan Kusini, Salva Kiir Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Juba inatolewa wakati huu ambapo utawala wa Khartoum umeendelea kuishutumu Serikali ya rais Salva Kiir kwa kuendelea kuwafadhili kwa silaha waasi wa jimbo la Darfur wanaopigana na Serikali.

Hapo jana rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amesema nchi yake itaendelea kuheshimu makubaliano ya amani waliotia saini na kukanusha nchi yake kuwa na uhusiano wowote na makundi ya waasi wa SPLM-N na JEM wanaopigana na Serikali ya Khartoum jimboni Darfur na Kordofan Kaskazini.

Kauli ya rais Kiir ilitiliwa mkazo wa waziri wa habari nchini humo Barnaba Marial Benjamin ambaye amesema wako tayari kuingia kwenye mazungumzo mapya na Khartoum kwa lengo la kujaribu kuwashawishi waasi kuacha kusonga mbele.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaona kuwa Serikali ya Khartoum haiwezi kulifunga bomba hilo kwakuwa nchi zote mbili zinategemea kwa sehemu kubwa mapato yanayotokana na biashara ya mafuta.

Nchi ya Sudan inasisitiza kuwa na ushahidi kuonesha Serikali ya Juba inawafadhili waasi wa Darfur ambao wameapa kuuangusha utawala wa rais Bashir.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanaona tuhuma za Sudan zina ukweli kutokana na ukweli ya kwamba makundi yote mawili yalipigana pamoja na rais Kiir katika kutafuta uhusuru wa Sudan Kusini na kwamba kiongozi huyo hawezi kuwasaliti wenzake.