PARIS-UFARANSA

Polisi nchini Ufaransa wamkamata mtuhumiwa wa kumshambulia mwanajeshi

Polisi wa Ufaransa wakilinda eneo ambalo mwanajeshi wake alichomwa kisu mwishoni mwa juma
Polisi wa Ufaransa wakilinda eneo ambalo mwanajeshi wake alichomwa kisu mwishoni mwa juma Reuters

Polisi nchini Ufaransa inamshikilia mtu mmoja mwenye umri wa miaka 22 kwa tuhuma za kuhusika na kumjeruhi mwanajeshi jijini Paris mwishoni mwa juma lililopita akituhumiwa kuwa mfuasi wa itikadi kali za kiislamu. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Manuel Valls amedhibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo siku ya jumatano magdharibi mwa nchi hiyo kwenye mkoa wa Yvelines.

Valls amesema kuwa mtuhumiwa huyo sasa yuko chini ya mahojiano na polisi maalumu wa kupambana ugaidi ambapo anadaiwa mwishoni mwa juma lililopita alimvamia mwanajeshi mmoja na kumchoma kisu shingoni.

Shambulio hilo lilitekelezwa wakati watu wakiwa kwenye shughuli zao za kawaida tukio lililojiri saa chache baada ya kuuawa kwa mwanajeshi mmoja wa Uingereza mjini London na watu wanaodaiwa kuwa wenye msimamo mkali wa dini ya Kiislamu.

Taarifa ya wizara inasema kuwa bado inafanyia uchunguzi tukio hilo kubaini iwapo mshukiwa aliyekamatwa anauhusiano wowote na watuhumiwa wa mjini London Uingereza ama anahusika na kupanga njama hizo za kushambulia wanajeshi.

Uchunguzi wa awali wa polisi unaonesha kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa amekuwa akijihusisha na harakati za makundi ya waislamu wenye msimamo mkali nchini humo na kwamba huenda akawa ametekeleza shambulio hilo akilenga kutuma ujumbe kwa Serikali ya Ufaransa.

Taarifa hoyo imeongeza kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa ni kijana ambaye hivi karibuni alitangaza kubadili dini na kuanza kufanya harakato za kuwatetea waislamu karibu miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo polisi wamekiri kuwa mtuhumiwa huyo hana rekodi zozote za uhalifu na kwamba hizi ni hatua za awali kuelekea kubaini ukweli hasa wa yeye kutekeleza shambulio hilo.