DRC-TANZANIA-RWANDA

Serikali ya DRC yapongeza kauli ya rais wa Tanzania kuhusu Rwanda

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC imepongeza kauli iliyotolewa na rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU kuhusu hali ya amani mashariki mwa nchi hiyo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda akisalimiana na rais wa Tanzania,  Jakaya Kikwete walipokutana kwenye moja ya mikutano yao
Rais Paul Kagame wa Rwanda akisalimiana na rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete walipokutana kwenye moja ya mikutano yao Reuters
Matangazo ya kibiashara

Rais Kikwete akifanya mahojiano na kituo cha kimataifa cha Ufaransa, RFI alinukuliwa akimtaka rais wa Rwanda Paul Kagame kufanya mazungumzo na wapiganaji waasi wa kundi la FDLR ili kupata suluhu kati yao.

Kauli ya rais Kikwete aliitoa wakati alipoulizwa kuhusu hatua ambazo zimepigwa na nchi za ukanda wa maziwa makuu ICGLR kuhusu kusaka amani ya kudumu nchini DRC na kusema kuwa makundi ya waasi wanaopigana na serikali ya Rwanda na ya Uganda ni lazima wakutanishwe na Serikali.

Mratibu wa ufuatiliaji wa mkataba uliotiwa saini mjini Addis Ababa Ethiopia kuhusu mpango wa amani wa DRC, Francois Mwamba, amepongeza msimamo wa rais wa Tanzania na kuongeza kuwa viongozi wengine wa Afrika wanapaswa kuiga mfano wake.

Mwamba ameongeza kuwa rais Kikwete ameonesha ujasiri na kutomwogopa mtu kuhusu suala la amani ya mashariki mwa DRC ambapo ameona kuna haja ya makundi ya waasi wa Rwanda na Uganda kuketi meza moja na Serikali zao kumaliza tofauti zao.

Katika hatua nyingine nchi ya Rwanda imekosoa vikali kauli ya rais Kikwete na kudai kuwa haiko tayari kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR ambao wanatuhumiwa kutekeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Rwanda.

Kauli hiyo pia ilipingwa na wanyarwanda wanaoishi nchini Marekani ambao wamemwandikia barua rais Barack Obama wakimataka amshinikize rais Kikwete kufuta usemi wake kuhusu waasi wa FDLR.

Nchi ya Tanzania ni kati ya mataifa ya ukanda wa maziwa makuu ambayo imetangza kupeleka wanajeshi wake zaidi ya elfu moja mashariki mwa DRC kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa UN wa kuunda kikosi maalumu kitakachokabiliana na waasi wa masharki mwa DRC.