AU

Viongozi wa Afrika wamefanikiwa kwenye mkakati wa uundaji kikosi cha dharura cha Afrika

Ikiwa siku mbili zimepita toka viongozi wa Umoja wa Afrika AU wamalize mkutano wao mjini Addis Ababa Ethiopia, wachambuzi wa masuala ya usalama wanaona kuwa viongozi hao wameshindwa kuja na mpango mkakati wa kiusalama barani Afrika.

Wanajeshi wa DRC wakiwa kwenye moja ya mazoezi ya kijeshi
Wanajeshi wa DRC wakiwa kwenye moja ya mazoezi ya kijeshi Reuters
Matangazo ya kibiashara

Licha ya viongozi hawa kukubaliana kuhusu kuundwa kwa kikosi cha dharura kitakachojumuisha wanajeshi zaidi ya elfu 32, bado wamekosolewa kutokana na kushindwa kuweka utaratibu ambao utafanikisha kupatikana kwa wanajeshi hao licha ya kwamba baadhi ya nchi zimeahidi kutoa wanajeshi wake.

Ni kanda tano tu za bra la Afrika ambazo zimefanikiwa kuunda jeshi la pamoja ambalo mara kadhaa limeshuhudiwa likitekeleza operesheni zake kikamilifu kwenye mataifa yao hasa jeshi la ECOWAS.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kushindwa kwa viongozi hao kuja na mkakati maalumu wa kuhakikisha kunaundwa kwa jeshi la dharura kutafanya kuchelewa kuchukua hatua stahiki kwenye maeneo ya vita.

Viongozi hao walikosolewa vikali kuhusu kushindwa kuchukua mapema dhidi ya makundi ya waasi kaskazini mwa Mali mpaka pale wanajeshi wa Ufaransa walipoingilia kati.

Mkuu wa tume ya usalama wa Umoja wa Afrika AU, Ramtane Lamamra amedhibitisha marais kukubaliana kuhusu kuundwa kwa kikosi maalumu cha dharura na kwamba wanafanyia kazi mpango huo ili kuhkikisha kuwa unaanza kufanya kazi.

Francis Onditi ni mchambuzi wa masuala ya siasa akiwa mjiniĀ Nairobi nchini Kenya na yeye anasema kuwa swali la kujiuliza hapa ni lini kikosi hicho kitaundwa na kwakiasi gani nchi wanachama ziko tayari kuchangia wanajeshi?

Mchambuzi huyu ameongeza kuwa ili kikosi hicho kiweze kufanya kazi ni lazima suala la namna ya kupata fedha za kuendesha operesheni zake liwekwe wazi na kwamba ni jukumu la mataifa yote kuchangia kwenye kikosi hicho.

Nchi za Ethiopia, Afrika Kusini na Uganda tayari zimetangaza utayari wake wa kutoa wanajeshi kwenye kikosi cha muda ambacho kitaundwa na umoja huo na kwamba michango ni ya hiari.