WHO-UN

WHO: Uzito uliopindukia ni hatari kwa afya, dunia yatakiwa kuchukua hatua

Unene uliopindukia ni chanzo cha magonjwa mengine kama ya moyo na saratani
Unene uliopindukia ni chanzo cha magonjwa mengine kama ya moyo na saratani Reuters

Shirika la afya duniani WHO limeonya dunia dhidi ya kuendelea kuongezeka kwa tatizo la watu kuwa na uzito kupita kiasi na kutaka hatua zaidi kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na shirika hilo zinaonesha kuwa karibu asilimia 70 ya watu wazima duniani wanakabiliwa na tatizo la uzito uliopitiliza na kwamba tatizo hilo linaanza kushuhudiwa hasa kwenye mataifa ya bara la Afrika na Latin Amerika.

Takwimu za WHO zinaitaja nchi ya Marekani kukithiri kwa kuwa na watu wengi wenye tatizo la uzito kutokana na kuongezeka kwa pato la nchi ambalo linawezesha watu kununua vyakula vinavyochangia tatizo hilo.

Hapo jana nchi wanachama za Umoja wa Mataifa UN, kwa kauli moja zilipitisha maazimio rasmi ya kupambana na tatizo la uzito ulopindukia, saratani, magonjwa ya moyo na kisukari.

Azimio hilo linazitaka nchi wanachama kuwa na mpango maalimu kwa kupambana na magonjwa hayo ambayo katika siku za hivi karibuni yamekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo kutokana na kuwakumba hata watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka 18.

Katika maazimio hayo yanataka nchi wanachama kutunga sheria ya kutoza kodi kwenye vyakula na juisi ambazo zinachangia kuongeza uzito hatua itakayosaidia wananchi kupunguza matumizi yake.

Baadhi ya nchi zinaona kuongezwa kwa kodi kwenye bidhaa za aina hiyo kutwafanya watumiaji kupunguza matumizi yake na kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la watu kuwa na uzito uliopindukia.