NIGERIA

Boko Haram: Hatujashindwa vita dhidi ya Serikali ya Nigeria

Sehemu ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria
Sehemu ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria Reuters

Wapiganaji wa kundi la kiislamu la Boko Haram nchini Nigeria wamesema kuwa licha ya mashambulizi ya vikosi vya Serikali kutaka kuwasambaratisha bado wao hawajashindwa vita hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye taarifa yao waliyoitoa kwa mara ya kwanza toka kuanza kwa opereseheni za kijeshi kwenye miji mitatu iliyotangaziwa hali ya hatari nchini humo, kundi hilo linadai kuwa operesheni ya Serikali inashindwa na kwamba wao ndio wataibuka washindi.

Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia mkanda wa video na kusomwa na kiongozi wa kundi hilo, Abubakar Shekau amewataka wafuasi wa kundi lake kutokatishwa tamaa na matamshi ya Serikali na kuwataka wananchi zaidi kujiunga na kundi lao.

Kundi hilo pia limeonesha picha za video zikionesha miili inayodai ni wanajeshi wa Serikali ambao iliwakamata wakiwa na magari yao kwenye majimbo ambayo wamekuwa wakikabiliana na wapiganaji hao.

Shekau amekejeli namna ambavyo jeshi la Nigeria linaendesha peresheni hiyo akidai kuwa wanajeshi wake wengi wamekuwa wakikimbia kupigana nao na kutupa silaha zao jambo linaloashiria ushindi kwa wapiganaji wake.

Kundi hilo pia limetaka waislamu nchini humo kujiunga kwenye vita waliyoita takatifu ya kupigania ukombozi wa taifa hilo ambao wao wanataka liwe taifa la kiislamu.

Toka kutangazwa kwa hali ya hatari May 14 na rais Goodluck Jonathan kwenye miji mikubwa mitatu nchini humo, Serikali imeeleza kufanikiwa kwenye vita dhidi ya wapiganaji hao na kwamba karibu asilimia 80 wamewatokomeza.

Maelfu ya wanajeshi wameongezwa kwenye operesheni hiyo ambapo Serikali inasema inalenga kuwaongezea nguvu wanajeshi waliokuwepo hapo awali ili kukabiliana na wapiganaji wa Boko Haram.

Hata hivyo jeshi la Nigeria limejikuta likikosolewa kwa sehemu kubwa kwa kile mashirika ya kutetea haki za binadamu wanasema kuwa wanajeshi wa Serikali wanashiriki vitendo vya ukiukaji haki za binadamu ikiwemo kuwakamata watu bila ya makosa pamoja na kuwadhalilisha wanawake.