CANADA-ERITREA

Canada yamfukuza nchini mwake balozi wa Eritrea, ni baada ya kukiuka vikwazo vya UN

Waziri wa mambo ya nje wa Canada, John Baird
Waziri wa mambo ya nje wa Canada, John Baird Reuters

Serikali ya Canada imetangaza kumfukuza nchini mwake balozi wa ritrea nchini humo pamoja na kufunga ubalozi wake kutokana na balozi huyo kukaidi vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa kwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa Canada kumfukuza nchini mwake balozi wa Eritrea unakuja kufuatia onyo lake la awali kwa balozi huyo kumtaka kutoomba fedha toka kwa rais wake wanaoishi nchini Canada kwa lengo la kusaidia jeshi la nchi hiyo.

Mwaka 2011 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN, lilipitisha azimio la kuiwekea vikwazo nchi ya Eritrea kwenye silaha na kupata msaada wa kifedha toka kwa raia wake wanaoishi ughaibuni.

Serikali ya Canada imemwandikia barua balozi wa Eritrea, Semere Ghebremariam Micael pamoja na maofisa wengine wa ubalozi huo kuondoka nchini huko mpaka kufikia tarehe 4 ya mwezi June.

Serikali ya Canada imesema kuwa mara kadhaa ilipata taarifa za balozi huyo kukiuka makataa iliyowekewa nchi yake na kuagiza uchunguzi kufanyika dhidi ya tuhuma hizo na kubaini kuwa alikiuka masharti ya Umoja wa Mataifa na nchi ya Canada kuhusu kuomba fedha kusaidia jeshi lake.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Canada, John Baird amesema kuwa uamuzi wa kuufunga ubalozi wa Eritrea umezingatia sheria za kimataifa na zile za nchi na kwamba kitendo hicho kisingeweza kuvumiliwa.

Nchi ya Eritrea iliwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa kufuatia tuhuma kuwa inashirikiana na wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia na kuhatarisha usalama wa tiafa hilo ambalo sasa lina Serikali mpya.