UGANDA

Hatimaye vituo vya habari vilivyofungwa nchini Uganda vyafunguliwa

Naibu mhariri mkuu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda (kushoto) Geoffrey Musana akimuangalia mlinzi wa ofisi hizo akifungua mlango wa kuingia ndani ya ofisi hizo
Naibu mhariri mkuu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda (kushoto) Geoffrey Musana akimuangalia mlinzi wa ofisi hizo akifungua mlango wa kuingia ndani ya ofisi hizo Reuters

Waziri wa mambo ya ndani wa nchi ya Uganda anayemaliza muda wake Hillary Onek hii leo ameagiza polisi nchini humo kuzifungua ofisi za vituo vya redio na magazeti ambavyo vilitangazwa kufungwa juma moja lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kampal, waziri Onek amesema ametoa maagizo kwa polisi kuondoka kwenye ofisi za gazeti la daily Monitor ambalo ofisi zake zilikuwa zimezungukwa kwa karibu siku kumi na moja.

Mbali na kuagiza polisi kuondoka kwenye ofisi za gazeti hilo, pia waziri ameagiza kuanza kazi kwa vituo vingine vya redio na magazeti zaidi ya kumi ambayo yalikuwa yamefungwa.

Juma moja lililopita, polisi nchini humo walivamia ofisi za gazeti la daily Monitor na vituo vyake mama vya redio KFM na Dembe FM na kuagiza kufungwa kutokana na kukataa kutoa ushirikiano na polisi.

Polisi walikuwa wakitafuta barua iliyochapishwa na gazeti hilo kutoka kwa aliyekuwa mkuu wa usalama wa taifa Jenerali David Sejusa akieleza mpango wa rais Museveni kumuandaa mtoto wake kurithi madaraka yake pindi akimaliza muhula wake.

Barua ya Sejusa ilimtaja mtoto wa Museveni, Brigedier Muhoozi Keinerugaba kuandaliwa na baba yake kuwa kiongozi wa majeshi na baadae kuchukua madaraka ya urais.

Barua hiyo pia ilianisha mpango wa Serikali kupanga njama za kutaka kuwaua maofisa wa juu wa jeshi la Uganda ambao wamekuwa wakimpinga rais Museveni na sera yake ya kutaka kumuandaa mtoto wake awe mtawala baada ya yeye kuondoka madarakani.

Kufungwa kwa vituo hivyo vya Redio na magazeti kuliamsha hisia toka kwa makundi ya wanaharakati ambapo walitaka Serikali kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.

Hata hivyo ofisi za gazeti binafsi la Red Paper zenyewe zitaendelea kusalia zimefungwa kwa kile ambacho Serikali bado haijatoa sababu ya kufanya hivyo.

Mahakama kuu nchini Uganda pia iliagiza wahariri na waandishi wa habari wa vituo vilivyofungiwa kutoa barua inayotakiwa na polisi lakini vyombo hivyo vilikaidi maagizo hayo.

Jenrali Sejusa kwa sasa yuko uhamishoni nchini Uingereza ambako ameomba hifadhi kutokana na kuhofia maisha yake.