MALI-UFARANSA

Maandamano zaidi yashuhudiwa nchini Mali kupinga kauli ya rais wa Ufaransa

wanajeshi wa Ufaransa wakiwa kwenye mji wa Kidal hivi karibuni, wanajeshi hao wanalinda uwanja wa ndege wa Kidal
wanajeshi wa Ufaransa wakiwa kwenye mji wa Kidal hivi karibuni, wanajeshi hao wanalinda uwanja wa ndege wa Kidal Reuters

Maelfu ya wananchi wa Mali kwenye miji mbalimbali nchini humo wameandamana kupinga mpango wa rais wa Ufaransa Francois Holande kuhusu utawala wa jimbo la Kidal kaskazini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Maandamano haya yanakuja wakati huu ambapo taifa la Mali linajiandaa na uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi July mwaka huu huku kukiwa na hofu kuhusu kufanyika kwa uchaguzi ulio uru na haki kwenye mji wa Kidal ambao unakaliwa na wapiganaji wa MNLA.

Maelfu ya vijana na wanawake kwenye mji wa Gao wameonekana wakiwa na mabango yanayosema hakuna uchaguzi bila ya kuamiana huku wakikashifu mpango wa rais Hollande kuhusu utawala wa Kidal wakimpongeza kwa kuleta amani lakini wakataka haki itendeke.

Hivi karibuni rais Francois Hollande alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa nchi yake itahakikisha jimbo la Kidal linakuwa chini ya mamlaka inayotambulika na sio waasi wa MNLA ambao wanataka kuwa na mamlaka rasmi kwenye mji huo.

Kauli ya Hollande imekuja kufuatia tangazo la kundi la MNLA kudai kuwa halitakubali wanajeshi wa Serikali kuingia kwenye mji huo na kuwa watawala wakati wao wana haki zote jambo ambalo liliibusha mvutano kati ya MNLA na upande wa Serikali.

Licha ya kundi la MNLA kusisitiza kuwa litaandaa uchaguzi wake Serikali ya Mali imesisitiza jimbo hilo kurejeshwa kwenye himaya yake na litafanya uchaguzi unaosimamiwa na Serikali nchi nzima.