MADAGASCAR-AU-UN

Serikali ya mpito ya Madagascar yatangaza kusogeza mbele tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu

Serikali ya mpito ya Madagascar imetangaza kuahirisha zoezi la uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi July mwaka huu baada ya mahakama kuu kubaini kuwa uchaguzi huo umeingiliwa na mataifa ya nje.

Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina
Rais wa Madagascar, Andry Rajoelina Reuters
Matangazo ya kibiashara

Taarifa iliyotolewa na Serikali, iliiagiza tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo CENIT kuahirisha zoezi la uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 24 ya mwezi July kwakile ilichoeleza kuwa kuna watu wamepanga njama kutaka kuharibu uchaguzi huo.

Taarifa hiyo ya Serikali bila ya kutaja mtu, kikundi wala taifa ambalo linahusishwa na kuingilia mchakato wa maandalizi ya uchaguzi huo, imesema kuwa hatua hiyo inalenga kutoa fursa ya kushughulikia matatizo yaliyoanza kujitokeza.

Ripoti ya Serikali inasema kuwa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni umebaini kuwa kuna mataifa ambayo yamekuwa yakifadhili baadhi ya vyama vya siasa nchini humo na makundi ya wanaharakati kwa lengo la kuingilia mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Uamuzi huo wa Serikali ulitangazwa pia na rais wa mpito aliyeingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2009, ametaka zoezi hilo kusogezwa mbele kwa mwezi mmoja kujiandaa zaidi.

Rais Rajoelina pia amekataa kujiuzulu nafasi yake miezi miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa kile ambacho anadai ni njama za kutaka kuipindua Serikali yake na kuharibu uchaguzi mkuu.

Hivi karibuni rais Rajoelina alitangaza kuwania nafasi ya urais pamoja na mke wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo marck ravalomanana, Lalao Ravalomanana hatua ambayo imerudisha nyuma juhudi za kupayikana kwa amani nchini humo.

Umoja wa Afrika AU umekataa kutambua uteuzi wake pamoja na ule wa mke wa Ravalomanana kwakuwa wao kwa kauli moja walikubaliana na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kutowania nafasi yoyote ya urais kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Miongozi mwa viongozi wengine ambao wanapingwa kuwania kiti cha urais ni rais wa zamani aliyerejea nchini humo Didier Ratsiraka.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amezitaka pande zinazozozana nchini humo kuketi meza moja kumaliza tofauti zao pamoja na kuwataka viongozi wote watatu kuondoa majina yao kwenye kinyang'anyiro hicho.