TANZANIA

Tanzania yatoa msimamo wake kuhusu nchi zenye migogoro barani Afrika

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernad Membe
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernad Membe Reuters

Nchi ya Tanzania yasema migogoro kwenye mataifa ya bara la Afrika la mashariki ya kati itatatuliwa kwa njia ya mazungumzo kuliko kutumia nguvu kuondoa Serikali halali madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Tanzania, Bernad Camilius Membe wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014 bungeni mjini Dodoma.

Akizungumzia mzozo wa mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, waziri Membe amesema nchi yake inaungana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kusaka amani ya mashariki mwa nchi hiyo na ndio maana ikapeleka wanajeshi wake huko kukabiliana na makundi ya waasi.

Waziri Membe ameongeza kuwa ni jukumu la nchi wanachama za ukanda wa maziwa makuu kuhakikisha usalama unarejea mashariki mwa nchi hiyo na kwamba Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.

Akizungumzia mzozo kati ya Sudan na Sudan Kusini kwenye maeneo ya mpakani na machafuko ya jimbo la Darfur, waziri Bernad Membe amesema kuwa chini ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika Tanzania itashiriki katika Kusaidia kupatikana kwa suluhu kwenye maeneo ya mpaka pamoja na kujaribu kuwashawishi waasi kufanya mazungumzo na Serikali ya Khartoum.

Kuhusu hali ya kisiasa nchini Madagascar, waziri Membe ameeleza Serikali ya Tanzania kusikitishwa na mwenendo wa kisiasa nchini humo kwa kile alichodai ni ukaidi wa viongozi mahasimu kutekeleza mapendekezo ya kupatikana kwa suluhu ya kisiasa.

Waziri Membe amongeza kuwa kitendo cha mke wa rais wa zamani Lalao Ravalomana na kutangaza kuwania urais ndiko kulikomfanya rais wa sasa Andry Rajoelina nae kubadilisha uamuzi wake na kutangaza kuwania urais.

Kuhusu mapinduzi yanayoendelea kuhsuhudiwa kaskazini mwa bara la Afrika, waziri Membe amesema hawaungi mkono njia za kimabavu kuingia madarakani na kwamba ni kwa njia ya uchaguzi mkuu pekee ndiyo kutapatikana kwa amani na demokrasia ya kweli.

Kuhusu suala la Syria, Serikali ya Tanzania imekosoa hatua ya nchi za Marekani, Uingereza na jumuiya ya Umoja wa Ulaya EU kuwaunga mkono waasi wa Syria na kutaka kutumia nguvu kuiondoa madarakani Serikali ya rais Bashar al-Assad.