IRAQ

UN yaonya dhidi ya mashambulizi ya kidini yanayoongezeka nchini Iraq

Mashambulizi mapya nchini Iraq yaliyotekelezwa hii leo kwenye maeneo mbalimbali ya mji wa Baghdad yameua watu nane na kujeruhi wengine zaidi ya 50, na kufanya idadi ya watu waliokufwa kwa wiki hii peke yake kufikia 160.

Moja ya mashambulizi yaliyotekelezwa juma hili nchini Iraq
Moja ya mashambulizi yaliyotekelezwa juma hili nchini Iraq Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi haya ni mfululizo wa vurugu za kidini zilizoibuka nchini humo kati ya waumini wa madhehebu ya Kisunni na kishia ambao wanapigania kuwa na madaraka sawa nchini humo.

Shambulizi hili linatekelezwa wakati huu ambapo waziri mkuu wa Nuri al-Maliki ametangaza wanajeshi wake kuwasaka watu wanaohusika na kupanga mashambulizi hayo.

Makundi ya watu wa madhehebu ya Kishia na Kisunni wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi ambapo safari hii misikiti ya Kishia imekuwa ikilengwa kwenye mashambulizi haya mapya.

Umoja wa Mataifa UN umetoa wito kwa viongozi wa Iraq kuharakisha mazungumzo ya pande zinazopigana nchini humo ili kunusuru machafuko hayo kuenea nchi nzima na badae kushindwa kutuliza ghasia hizo za kidini.

Umoja wa mataifa umeeleza hofu yake juu ya vurugu hizo na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe kukabiliana na makundi ya kigaidi ambayo yameanza kujipenyeza kutekeleza mashambulizi.

Hivi karibuni waziri mkuu Maliki alitangaza kufanyia mabadiliko makubwa sekta ya usalama nchini humo ambapo aliwabadilisha kazi maofisa wa juu wa usalama nchini humo hatua iliyolenga kuimarisha usalama nchini humo.

Shambulia la siku ya alhamisi lilitekelezwa kwa kutumia gari mjini Baghdad na kuua watu 4 kabla ya kutekelezwa kwa shambulio jingine kama hilo nje kidogo mwa mji wa Baghdad na kuua watu wawili na kujeruhi wengine zaidi ya 10.

Hapo jana mtu mmoja alijitoa muhanga kwenye sherehe moja ya kuzaliwa kusini mwa mji wa Baghdad na kuua watu 28 na kujeruhi wengine zaidi ya mia moja.

Mashambulizi haya yanafanya idadi ya watu waliokufa kwa mwezi wa tano pekee kufikia 580 huku idadi ya watu waliokufa katika miezi miwili iliyopita ikifikia elfu moja.