SYRIA-MAREKANI-URUSI-UTURUKI

Shehena ya kwanza ya silaha toka Urusi yawasili Syria, upinzani watoa masharti kushiriki mazungumzo ya amani

Miongoni mwa silaha za Urusi ambazo zimepelekwa nchini Syria kusaidia kulinda usalama wake dhidi ya uvamizi wa mataifa ya nje
Miongoni mwa silaha za Urusi ambazo zimepelekwa nchini Syria kusaidia kulinda usalama wake dhidi ya uvamizi wa mataifa ya nje Reuters

Upinzani nchini Syria ambao wanaendelea na mkutano wao mjini Instanbull, Uturuki wametangaza masharti mapya ya kutekelezwa kabla ya wao kuingia kwenye mkutano wa kimataifa wa amani kuhusu Syria uliopangwa kufanyika mwezi ujao mjini Geneva.

Matangazo ya kibiashara

Viongozi wa muungano wa baraza la upinzani nchini Syria wanatarajiwa kukutana alhamisi ya wiki hii kutazama namna bora zaidi ya wao kluweza kushirikia mazungumzo hayo yaliyoandaliwa na Serikali za Marekani na Urusi.

Miongoni mwa mambo ambayo upinzani unataka yatekelezwe kabla ya kuingia kwenye mazungumzo hayo ni pamoja na rais wa Syria Bashar al-Assad kujiuzulu ndipo wao waingie kwenye mazungumzo.

Matakwa haya ya upinzani yanakuja wakati huu ambapo Serikali ya rais Assad juma hili ilitangaza utayari wake wa kushiriki kwenye mazungumzo hayo bila ya kuweka masharti yoyote ikiwa ni mkutano wao wa kwanza upinzani kukutana uso kwa uso na utawala wa Assad.

Kwenye taarifa yao waliyoitoa mjini Instanbull, imesema kuwa wao wanaunga mkono juhudi za mataifa ya magharibi lakini hawawezi kushiriki kwenye mazungumzo hayo iwapo rais Assad ataendelea kubakia madarakani.

Taarifa hiyo pia imepongeza uamuzi uliofikiwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya kuwaondolea vikwazo vya silaha waasi wa Syria na kuongeza kuwa kufanya hivyo kutasaidia wapiganaji hao kusonga mbele kuelekea Damascus.

Mbali na kupongeza hatua ya Umoja wa Ulaya, upinzani umekosoa mpango wa Serikali ya Urusi kutaka kupeleka Silaha zaidi kwa Serikali ya Assad jambo ambapo pia kwenye makataa yao wanatakaUrusi isitekeleze mpango wake huo iwapo waasi wanataka washiriki kwenye mkutano huo.

Katika hatua nyingine rais Assad akihojiwa na kituo cha televisheni cha Hezebollah amedhibitisha kuwasili kwa meli ya kwanza iliyosheheni silaha toka nchini Urusi chini ya makubaliano waliyotiliana saini kuimarisha usalama wake.

Utawala wa Assad pia umesema na wao hawatakuwa tayari kushiriki mazungumzo ya kimataifa ya amani mjini Geneva iwapo upinzani utatoa masharti ya aina yoyote kwa wao kuweza kushiriki kwenye mazungumzo ya amani.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa matakwa ya upinzani haya msingi wowote kwa sasa kwakuwa hii ni nafasi ya pekee kwa wao kukutana na Serikali kutafuta suluhu ya kudumu ya machafuko yanayoendelea nchini Syria.