MYANMAR-KACHIN

Waasi wa Kachin na Serikali ya Myanmar wakubaliana kusitisha mapigano

Kiongozi wa waasi wa kundi la Kachin akizungumza na mwenzake toka jeshi la Serikali ya Myanmar
Kiongozi wa waasi wa kundi la Kachin akizungumza na mwenzake toka jeshi la Serikali ya Myanmar Reuters

Serikali ya Myanmar na waasi wa Kachin kaskazini mashariki mwa nchi hiyo hatimaye wamefikia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa karibu miaka miwili na kutoa matumaini ya kupatikana kwa amani kwenye jimbo la Kachin.

Matangazo ya kibiashara

Msuluhishi mkuu wa wa mzozo wa jimbo la Kachin, Min Zaw Oo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa waasi wa Kachin na upande wa Serikali wamekubaliana kutia saini makuliano ya awali yanayolenga kumaliza mapigano jimboni humo.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, tayari wamekubaliana mambo saba ya kutekeleza ili kufikia malengo ya kupatikana kwa suluhu huku kubwa likiwa ni kusitishwa kwa mapigano yoyote kati ya waasi wa vikosi vya Serikali.

Zaw Oo ameongeza kuwa baada ya pande hizo mbili kutiliana saini, kinachofuata sasa ni kuwa na mazungumzo ya kina yatakayohusisha wanajeshi wa serikali na waasi kukubaliana namna ya kuondoa wapiganaji wao kwenye maeneo ambayo yameshuhudia mapigano.

Waasi wa Kachin na rais wa Myanmar, Thein Sein wamekuwa na mazungumzo kwenye mji wa Myitkyina ambao ni makao makuu ya jimbo la Kachin kwa muda wa siku tatu mazungumzo ambayo hatimaye yameza matunda.

Mazungumzo kama haya yaliwahi kufanyika mpakani na nchi ya China lakini hata hivyo hayakuweza kufua dafu baada ya pande hizo mbili kushindwa kufikia makubaliano ya kumaliza machafuko.

Maelfu ya wananchi wa jimbo la Kachin wameyakimbia makazi yao toka mwaka 2011 mwezi June wakati mkataba wa amani uliodumu kwa miaka 17 ulipovunjika na kuzuka kwa mapigano mapya.

Mapigano baina ya wanajeshi wa Serikali na waasi wa Kachin pamoja na vurugu za kidini zinazoendelea kushuhudiwa nchini humo zimechangia kuharibu mabadiliko ya kidekorasia ambayo yalianza kushuhudiwa toka kuingia madarakani kwa utawala wa kiraia.

Waasi wa Kachin nashinikiza serikali ya Myanmar kuwapa nafasi zaidi ya kushiriki kwenye siasa za nchi yao.