SYRIA-MAREKANI-URUSI-ISRAEL

Assad: Syria itajibu mashambulizi dhidi ya Israel, Urusi yasisitiza misaada zaidi ya silaha kwa Serikali yake

Rais wa Syria Bashar al-Assad ameapa nchi yake kujibu mashambulizi ya aina yoyote mapya yatakayofanywa dhidi yake na nchi ya Israel wakati huu ambapo mapigano mapya yameripotiwa kwenye mji wa Golan.

Rais wa Syria Bashar al-Assad akifanya mahojiano na kituo cha televisheni cha el-Manar
Rais wa Syria Bashar al-Assad akifanya mahojiano na kituo cha televisheni cha el-Manar REUTERS/SANA
Matangazo ya kibiashara

Akifanya mahojiano na kituo cha televisheni cha Al-Manar, rais Assad amesema kwa sasa nchi yake haitokaa kimya tena iwapo Israel itafanya mashambulizi dhidi yake na kwamba majeshi yake yatalazimika kujibu mapigo.

Rais Assad pia amesema anashukuru wapiganaji wa vuguvugu la Hezbollah la nchini Lebanon kwa kuendelea kumuunga mkono kwenye vita dhidi ya makundi aliyiyaita ya kigaidi.

Kiongozi huyo akaongeza kuwa kwa sasa nchi ya Urusi imeahidi kuendelea kuisaidia nchi yake kwa silaha zaidi ya kijeshi kuweza kukabiliana na uasi ambao unaendeshwa na upinzani kwa jina la Mungu na kwamba awamu ya kwanza ya silaha iliyowasili itasaidia kwa sehemu kubwa kushinda vita hivyo.

Rais Assad ameendelea kuyakosoa mataifa ya magharibi kwa kuendelea kuwapatia silaha waasi wa Syria, silaha ambazo amesema zinaishia kwenye makundi ya kigaidi ambayo sasa yanazidi kukita mizizi na kuwa tishio sio tu kwa nchi yake lakini hata kwa mataifa ya magharibi.

Marekani na Uingereza zimekosoa mpango wa Urusi kuendelea kuusaidia utawala wa Assad na kwamba kufanya hivyo kutafanya vita hivyo kuendelea mpango ambao Urusi nao inakosoa mataifa hayo kwa kuwaondolea vikwazo vya silaha makundi ya waasi.

Hapo jana baraza la taifa la muungano wa upinzani nchini Syria lilitangaza kutoshiriki mazungumzo ya amani yaliyoandaliwa na Urusi na Marekani kwa kile walichodai watafanya hivyo iwapo wapiganaji wa Hezbollah wataondoka kwenye mji wa Quasry.