KENYA

Mahakama kuu ya Kenya kusikiliza kesi dhidi ya kuvunjwa kwa tume ya mishahara

Mahakama kuu jijini Nairobi inatarajiwa kusikiliza hoja ya kutaka kuvunjiliwa mbali kwa tume ya kutathmini mishahara ya watumishi wa umma nchini Kenya, hoja ambayo iliwasilishwa mahakamani na spika wa bunge la kaunti ya embu Justin Mate.   

Baadhi ya waandamanaji na wanaharakati walioandamana nje ya ofisi za bunge la Kenya hivi karibuni
Baadhi ya waandamanaji na wanaharakati walioandamana nje ya ofisi za bunge la Kenya hivi karibuni RFI
Matangazo ya kibiashara

Haya yanajiri huku wabunge nchini Kenya wakipanga kupunguza mshahara wa rais kwa asilimia 57, kando na kupunguza kiwango cha ushuru kinachotozwa wakenya.

Hivi karibuni wabunge nchini humo walidai kuwa tume ya marekebisho ya mishahara nchini humo haina mamlaka ya kubadili wala kuunda sheria ambazo zilipitishwa na bunge na kutaka tume hiyo ivunjiliwe mbali.

Wabunge hao waliapa kuendelea kuishinikiza tume hiyo kurekebisha kiwango chao cha mshahara ama ikubaliane na kile ambacho kitaambuliwa na bunge ambalo ni juma hili tu wameidhinisha sheria ya kutaka tume hiyo ivunjwe ama ifanyiwe marekebisho.

Wabunge nchini Kenya wanataka nyongeza ya mshahara toka laki tano za Kenya wanazolipwa sasa hadi kufikia kiwango cha awali cha laki nane na nusu jambo ambalo tume ya marekebisho ya mishahara imesema haliwezekani.

Mbali na wabunge kutaka mishahara yao kufanyiwa marekebisho pia wanataka makamishan wa tume hiyo kupunguzwa kutoka tisa hadi watano.

Hatua ya wabunge kudai nyongeza kubwa ya mishahara iliibua hisia toka kwa wanaharakati na wananchi wa Kenya ambao wanaona kuwa wabunge wao watakuwa walafi iwapo wataongezewa mishahara huku wananchi wao wakiishi kimasikini.

Maandamano makubwa yalishuhudiwa nje ya bunge mwezi mmoja uliopita ambapo wanaharakati walidiriki hata kupeleka nguruwe nje ya geti la bunge kuonesha wabunge hao kuwa wanafanana na nguruwe kwakuwa hawajali kile wanachokula.

Katika hatua nyingine kumeibuka mvutano kati ya bunge kuu na lile la seneti ambapo wabunge wa bunge la juu wanataka bunge la seneti livinjwe kwakuwa halina kazi kubwa jambo ambalo limekanushwa vikali na wabunge wa seneti.