WHO-TOBACCO

WHO yazitaka nchi kupiga marufuku matangazo na kampeni za matumizi ya Tumbaku

Siku ya kimataifa ya kupiga vita matumizi ya Tumbaku
Siku ya kimataifa ya kupiga vita matumizi ya Tumbaku Reuters

Shirika la afya duniani WHO limezitaka serikali mbalimbali duniani kupiga marufuku matangazo yote kuhusu matumizi ya tumbaku, kampeni na udhamini kwenye shughuli mbalimbali za kijamii.

Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi wa shirika hilo, Douglas Bettcher amesema kuwa wakati umefika kwa serikali duniani kupiga marufuku matangazo yote ya tumbaku ambayo yanachochea watu kuwa na matumizi makubwa ya tumbaku ambayo inaathiri afya zao.

Ameongeza kuwa kufanya hivyo kutawafanya watu kupunguza matumizi ya tumbaku na hivyo kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu na maradhi mengine yanayotokana na utumiaji wa tumbaku.

Shirika hilo linasema kuwa kwa nchi ambazo tayari zimetunga na kupitisha sheria ya kupiga marufuku matangazo ya tumbaku zimefanikiwa kukabiliana na tatizo hilo kwa karibu asilimia 7.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon amezitaka nchi wanachama za Umoja wa Mataifa kutekeleza mapendekezo ya shirika la Afya WHO kutunga sheria zinazokataza matangazo ya tumbaku, kampeni zake na udhamini kwenye matukio mbalimbali.

Siku ya kimataifavya kupiga vita matumizi ya tumbaku huadhimishwa kila ifikapo tarehe 31 ya mwezi wa tano kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni kupiga marufuku matangazo, kampeni na udhamini wa makampuni yanayotengeneza bidhaa za tumbaku.