NIGER-MALI

Wafungwa 22 wakiwemo Magaidi wametoroka gerezani nchini Niger na kuwaua Askari watatu waliokuwa wanalinda eneo hilo

Gereza ambalo wafungwa 22 wametoka nchini Niger na kuwaua walinzi watatu waliokuwa kazini
Gereza ambalo wafungwa 22 wametoka nchini Niger na kuwaua walinzi watatu waliokuwa kazini AFP PHOTO / STRINGER

Serikali ya Niger imekiri wafungwa ishirini na wawili wametoroka gerezani baada ya kufanyika shambulizi lililochangia askari watatu kupoteza maisha baada ya wafungwa hao kujihami kwa silaha wakati wakifanya shambulizi lao.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa wafungwa hao ishirini na wawili waliotoroka wamo wale wanaotajwa kufungwa kwa makosa ya ugaidi huku serikali ya Niamey ikikiri magaidi waliotoroka ni hatari sana kwa usalama wa wananchi wa eneo hilo.

Waziri wa Sheria Marou Amadou ameviambia vyombo vya habari kwamba mmoja wa magaidi hatari waliotoroka ni pamoja na Cheibane Ould Hama kutoka nchini Mali anayetajwa kuwaua raia wanne kutoka Saudi Arabia na raia mwingine wa Marekani.

Amadou ambaye ni Kaimu Msemaji wa Serikali ya Niamey amesema Hama ni mtu hatari sana na wameanzisha msako kabambe wa kuhakikisha wanamtia nguvuni ili aendelee kutimikia adhabu inayomkabili.

Waziri Amadou ameongeza kuwa wafungwa wanaokabiliwa na makosa ya ugaidi ndiyo waliowaua askari watatu kwa kurushiana nao silaha ambazo bado hazijabainika walizitoa wapi na hata kufanikiwa kufanya shambulio hilo.

Tukio hili limekuja baada ya Makundi ya Wanamgambo wa Kiislam kufanya shambulizi nchini Niger kulenga kambi ya kijeshi pamoja na machimbo yanayomilikiwa na Ufaransa na kuchangia vifo vya watu zaidi ya ishirini.

Serikali ya Niger imejiapiza kuhakikisha inafanya msako ili kuwakamata wafungwa wote waliotoroka wakiamini watakuwa wamekwenda kujiunga na Makundi ya Wanamgambo wa Kiislam katika nchi hiyo.

Shambulizi hilo la gerezani na kuchangia kutoroka kwa wafungwa hao wanaotajwa ni magaidi limeleta hofu nchini Mali ambapo Jeshi limesema litachangia kuzorotesha mkakati wao wa kuyamaliza Makundi ya Kiislam.

Tukio hili linakuja kipindi hiki ambacho Serikali ya Mali ikiendelea kupambana na Makundi ya Kiislam ambayo yalikuwa yanashikilia eneo la Kaskazini mwa Taifa hilo kwa kipindi cha miezi kumi.