SYRIA-LEBANON

Wanamgambo wa Hezbollah waendelea kupambana na Wapiganaji wa Upinzani nchini Syria katika Mji wa Qusayr

Wapiganaji wakiendelea kushambuliana katika Mji wa Qusayr nchini Syria wakitumia njia za ardhini na hata angani
Wapiganaji wakiendelea kushambuliana katika Mji wa Qusayr nchini Syria wakitumia njia za ardhini na hata angani

Mapigano makali yameendelea kuutikisa Mji wa Qusayr nchini Syria kutokana na mashambulizi ya mabomu yanyofanywa baina ya Wapiganaji wa Upinzani wanaokabiliana na Wanamgambo wa Hezbollah kwa kipindi cha zaidi ya majuma mawili kipindi hiki watu tisa wakiuawa kwenye shambulizi la bomu la kujitoa mhanga Jijini Damascus.

Matangazo ya kibiashara

Ndege za kivita zimeonekana katika anga la Mji wa Qusayr zikishambulia kwa kutumia mabomu na kuchangia hali ya usalama kwa wananchi wanaoishi kuwa hatarini kipindi hiki Shirika la Msalaba Mwekundu Dunian ICRC likiomba mapigano hayo kusitishwa ili waweze kutoa msaada kwa waathirika.

Wanamgambo wa Hezbollah wameendelea kuwa mstari wa mbele kupambana na Wapiganaji wa Upinzani ambao wanataka kuiangusha Serikali ya Rais Bashar Al Assad huku wakipata uungwaji mkono kutoka Mataifa ya Magharibi.

Mapigano baina ya Wanamgambo wa Kundi la Hezbollah na Wapiganaji wa Upinzani nchini Syria yamekuwa yakiendeshwa katika eneo la mpaka wa Syria na Lebanon na kusababisha watu kukimbia makazi yao.

Taarifa zinasema Wapiganaji kumi na watano wa Upinzani wamepoteza maisha kwenye mapigano hayo huku Wanamgambo wa Hezbollah wakipoteza mwanachama wao mmoja huku wakifanikiwa kuweka kwenye himaya yao eneo la Bekaa.

Haya yanaendelea kipindi hiki Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC likinyosha kidole cha lawama kwa Urusi ambao wameituhumu kukwamishwa azimio linaloeleza hali mbaya ya Syria inachangia nchi hiyo kugeuka kaburi la wananchi wake.

Urusi imeendelea kuwa mtetezi imara na msaada mkubwa kwa serikali ya Rais Assad ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC huku wakiendelea kutoa silaha kwa serikali iweze kuendelea na mapigano hayo.

Katika hatua nyingine serikali ya Ufaransa imetoa pendekezo la kutakakusogezwa mbele kwa mazungumzo yaliyopangwa kufanyika nchini Uswiss katika Jiji la Geneva ukiwashirikisha wapinzani na serikali.

Ufaransa imetoa tamko hilo kutokana na machafuko yanayoendelea kukua katika nchi ya Syria kipindi hiki takwimu zinaonesha watu wapatao 94,000 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa machafuko yaliyodumu kwa karibu miezi ishirini na saba.