PAKISTAN-MAREKANI

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ataka Marekani kuacha kutumia ndege zisizo na rubani kufanya mashambulizi

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ambaye ametaka Marekani kuacha kutumia ndege zisizo na rubani kufanya mashambulizi
Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ambaye ametaka Marekani kuacha kutumia ndege zisizo na rubani kufanya mashambulizi REUTERS/Damir Sagolj

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ameitaka serikali ya Marekani kuacha mara moja kuendelea kutumia ndege zisizo na rubani ambazo zimekuwa zikitekeleza mashambulizi ya angani katika nchi hiyo na kuchangia mamia ya wananchi kupoteza maisha.

Matangazo ya kibiashara

Sharif ambaye ameapishwa kuendelea kuongoza Pakistan kwa awamu nyingine amesema wakati wa kusitishwa kwa mashambulizi hayo ya angani yanayotumia ndege za kivita umefika ili kunususru maisha ya wananchi wasio na hatia.

Tamko la Sharif linakuja kipindi hiki ambacho Bunge limepitisha sheria ambayo itazuia Waziri Mkuu kuongoza kwa vipindi vitatu na hivyo kunaonesha hiki kitakuwa kipindi cha mwisho kwa Waziri Mkuu.

Sharif amesema atafunga safari kwenda nchini Marekani kukutana na Rais Barack Obama ili aweze kumueleza msimamo wao juu ya matumizi ya ndege hizo zisizo na rubani zinazofanya mashambulizi Kaskazini Magharibi mwa Taifa hilo.

Waziri Mkuu Sharif amesema wao wanaheshimu sana utaifa wa kila nchi na wangependa pia maamuzi yaheshimiwe na mataifa mengine kwani kwa sasa wanataka matumizi ya ndege zisizo na rubani yafike mwisho.

Licha ya kauli hiyo Sharif ameendelea kutoa hakikisho la nchi yake kuwa tayari kushirikiana na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO ambayo yamekuwa kwenye mapambano dhidi ya Makundi ya wanamgambo.

Sharif ameitaka serikali ya Washington kuhakikisha inasimama kidete ili kumaliza muda wa operesheni yake dhidi ya makundi ya wanagambo ikiwemo Taliban na Al Qaeda ambayo imekuwa sababu ya kutumika kwa ndege hizo zisizo na rubani.

Mashambulizi ya hivi karibu yaliyotekelezwa nchini Pakistan kwa kutumia ndege zisizo na rubani yalichangia kuuawa kwa Naibu Kiongozi wa Taliban Waliur Rehman huku wananchi nao wakiuawa.

Waziri Mkuu Sharif amesema serikali yake ipo tayari kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Kundi la Wanamgambo wa Taliban wakiwa na lengo la kufikia suluhu ili kumaliza mapigano ya kila mara.

Sharif ambaye alishawahi kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka kumi na tatu akituhumiwa na serikali ya kijeshi alipanga kufanya mapinduzi ameapishwa na Rais Asif Ali Zardari kuongoza kwa awamu yake ya pili.