KOREA KASKAZINI-KOREA KUSINI

Serikali ya Korea Kaskazini yaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha jirani zao wa Korea Kusini wanafanya nao mazungumzo

Eneo la mpaka kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini linaloelekea katika Ukanda wa Viwanda wa Kaesong
Eneo la mpaka kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini linaloelekea katika Ukanda wa Viwanda wa Kaesong REUTERS/Lee Jae-Won

Serikali ya Korea Kaskazini imeendelea kusimama kidete kuhakikisha mazungumzo baina yao na jirani zao wa Korea Kusini yanafanikiwa na tayari imeshaanza kuchukua hatua madhubuti ili mpango wao ukamilike.

Matangazo ya kibiashara

Pyongyang katika kuonesha ipo tayari kurejesha uhusiano mzuri na jirani zao wa Seoul imetangaza pia kurejesha mawasiliano ya simu yaliyokatwa baada ya nchi hizo kuingia kwenye mgogoro mapema mwaka huu.

Ujumbe wa Pyongyang na ule wa Seoul ukiwajumuisha mawaziri unatarajiwa kuketi kwa mara ya kwanza tarehe 12 mwezi Juni ikiwa ni mwanzo waharakati za kuhakikisha mazungumzo zaidi yanafanyika.

Msemaji wa Serikali ya Korea Kaskazini amekiri wenzao wa Korea Kusini wameonesha wapo tayari kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kuhakikisha wanakuwa na uhusiano mzuri baina ya pande hizo mbili.

Korea Kaskazini na Korea Kusini almanusura ziingie kwenye vita baada ya Pyongyang kukerwa na hatua ya Seoul kufanya mazoezi ya kijeshi na Jeshi la Marekani hatua iliyooneka kuwa ni uchokozi kwao.

Mazungumzo haya yaliyopendekezwa na Pyongyang na kukubaliwa na Seoul yanatarajiwa pia kujadili hatua ya kufunguliwa kwa ukanda wa eneo la viwanda linalomilikiwa na pande hizo mbili la Kaesong.

Korea Kaskazini iliwatimua wafanyakazi wote kutoka Korea Kusini kuingia kwenye eneo hilo kwa kile ilichosema mataifa hayo yapo vitani kwa hiyo hairuhusu wageni kuvuka mpaka wao.

Serikali ya Pyongyang imejikuta kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa mataifa ya magharibi ikitakiwa kuachana na majaribio yake ya silaha za nyuklia ambayo wameendelea kuyafanya kwa makombora ya masafa marefu na mafupi.

Vikwazo na shinikizo hilo kwa Korea Kaskazini lilichangia nchi hiyo kutishia kushambulia Korea Kusini, Japana na kambi zote za Kijeshi za Marekani zinazopatikana kwenye eneo la Peninsula.

Marekani yenyewe imeendelea kusema Korea Kaskazini itapata ushirikiano kutoka Jumuiya ya Kimataifa iwapo itakuwa tayari kusitisha mradi wake wa majaribio ya silaha za nyuklia na kuacha kabisa kutengeneza silaha hizo.