MISRI-MORSI

Ghasia za kupinga kuondolewa madarakani Mohammad Morsi zazidi kushika kasi nchini Misri

REUTERS/Khaled Abdullah

Watu zaidi ya ishirini na sita wamekufa katika ghasia zinazoendelea kuchacha nchini Misri baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa madarakani Mohammad Morsi ambaye ni Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo. Wengi waliouawa ni wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood walioshiriki maandamano ya siku ya ijumaa wakilishinikiza jeshi kumrejesha madarakani Rais wao aliyekaa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee.

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa ya mapema jumamosi hii, wafuasi wa Muslim Brotherhood wameapa kuzidi kuendesha maandamano ya amani mpaka kiongozi wao atakaporejeshwa.

Morsi ambaye hajajitokeza kwa umma toka kupinduliwa, amewataka wafuasi wake kupigania haki yao kwa kiongozi waliyemchagua katika uchaguzi wa kidemokrasia.

Kwa upande wake jeshi limesisitiza kufanyika maandamano ya amani pekee wakati huu ambapo Rais wa mpito Adly Mahmud Mansour, akisema kuwa uchaguzi Mkuu utafanyika hivi karibuni ili kuwapa nafasi wananchi wa Misri kuamua ni nani wanayetaka awaongoze.

Taarifa toka nchini humo zimeeleza kuwa baadhi ya wanachama wa Muslim Brotherhood sambamba na Bwana Morsi watafikishwa mahakamani siku jumatatu kusomewa mashtaka ya kukiuka amri ya mahakama.

Tayari Umoja wa Afrika AU umesitisha uanachama wa Misri katika Umoja huo na kusema hautambui mapinduzi hayo kwa sababu Morsi alichaguliwa kidemokrasia baada ya kuondolewa kwa Rais wa zamani Hosni Mubarak.