Misri

Mwendesha Maashtaka nchini Misri aamuru kukamatwa kwa Viongozi wa Chama cha Muslim Brotherhood

Rais wa Misri, Mohamed Morsi, aliyepinduliwa na Jeshi
Rais wa Misri, Mohamed Morsi, aliyepinduliwa na Jeshi AFP PHOTO/KARIM SAHIB

Mwendesha Mashtaka nchini Misri ametoa amri ya kukamatwa kwa Kiongozi wa Chama cha Muslim Brotherhood Mohammed Badie na Viongozi wengine wa juu wa Chama hicho wakiwashutumu kuwa Chanzo cha Machafuko yaliyosababisha Maisha ya Watu kupotea.

Matangazo ya kibiashara

Takriban Watu 51 waliuawa kwenye Machafuko siku ya jumatatu nje ya Kambi kuu ya Jeshi jijini Cairo ambapo Wafuasi wa Kiongozi aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi wakitaka arudishwe madarakani walivamia eneo hilo.
 

Katika hatua nyingine Chama cha Muslim Brotherhood chakataa kupatiwa nafasi yeyote ndani ya Serikali ya mpito nchini Misri, badala yake kimesisitiza kurejeshwa madarkani kwa aliyekuwa Kiongozi wa taifa hilo,Mohamed Morsi.
 

Saa kadhaa baada ya kuteuliwa kwa Waziri Mkuu Maafisa nchini humo walitangaza kuwa Chama cha Muslim Brotherhood na chama cha kiislamu cha Nour vitapatiwa nafasi za uwaziri katika Serikali ya Mpito ya nchini Misri.
 

Hazem el-Beblawi, Mchumi na Waziri wa zamani wa Fedha ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Msemaji wa Ofisi ya Rais Ahmed al Muslimani ameeleza.
 

Mshindi wa Tuzo la amani la Nobel na Kiongozi wa Upinzani nchini Misri, Mohamed ElBaradei aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais katika wizara ya Maswala ya mambo ya nje.
 

Uteuzi huo ulifuatiwa na Tangazo kuwa nafasi za uwaziri katika Serikali mpya zitaachwa kwa Chama cha Freedom and Justice,Muslim Brotherhood na Nour.
 

Hatua ya uundwaji wa Serikali ya mpito imekuja takriban juma moja baada ya Jeshi kumuangusha aliyekuwa Rais wa Misri, Mohamed Morsi na kumteua Adly Mansour kuwa Rais wa nchi hiyo.
 

ElBaradei awali ilisemekana kuwa aliteuliwa kuongoza Baraza la Mawaziri lakini uteuzi wake haukuungwa mkono na Chama cha Nour.
 

Waziri Mkuu mpya anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuliunganisha Taifa lililogawanyika na kuunusuru Uchumi wa nchi hiyo.