CHINA

Marekani yaghadhabishwa na hatua ya China kushindwa kumkabidhi Snowden kwa Marekani

Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi nchini Marekani, Edward Snowden
Mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Kijasusi nchini Marekani, Edward Snowden youtube.com/screenshot RFI

Marekani imeiambia China kuwa imekasirishwa na hatua yake ya kutomkabidhi aliyekuwa Mfanyakazi wa Shirika la Kijasusi nchini Marekani, Edward Snowden baada ya kukimbilia nchini Hong Kong, ikisema kuwa kitendo hicho cha China kimeyumbisha uhusiano wao.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Marekani, Barrack Obama, alipokutana na Maafisa wa nchini China waliokuwa jijini Washington kwa ajili ya Mazungumzo ameeleza kusikitishwa na juu ya suala la Snowden, Ikulu ya Marekani imeeleza.
 

Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, William Burns mmoja kati ya Maafisa wa Marekani katika mazungumzo amesema Obama na Rais wa China, Xi Jinping walikubaliana walipokutana mwezi uliopita, kushirikiana wanapokutana na Changamoto mbalimbali.
 

Hiyo imeelezwa kuwa sababu ya kusikitishwa kwao na mamlaka ya Beijing na Hong Kong zilivyoshughulikia suala la Snowden ambayo, kwa mujibu wa marekani imeathiri jitihada za kujenga na kudumisha hali ya kuaminiana wakati maswala magumu yanapowakabili.
 

Snowden, alitorokea Hong Kong baada ya kutoa siri juu ya shughuli za kijasusi zinazofanywa na Marekani kwa njia ya Mtandao,Marekani nayo ikimsaka kwa ajili ya kujibu shutuma hizo.
 

Lakini Snowden aliondoka mjini Hong Kong, akiwa huru kabisa na kuelekea nchini Urusi.
 

Tangu kuwasili nchini Urusi tarehe 23 mwezi Juni, Snowden alikwama jijini Moscow katika Uwanja wa ndege nchini humo wakati akitafuta nchi ya kumpatia hifadhi.