MISRI-MORSI

Mwendesha mashtaka wa Misri aanzisha uchunguzi dhidi ya Rais aliyeondolewa madarakani

REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Ofisi ya mwendesha mashtaka nchini Misri imetangaza kuanziasha uchunguzi dhidi Mohamed Morsi, ambaye ni Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Taifa hilo na kuweka historia ya kukaa madarakani kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kukumbwa na mapinduzi ya kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya ofisi hiyo imeeleza kuwa imepokea malalamiko yanayomkabili Bwana Morsi, wanachama nane wafuasi wa Muslim Brotherhood akiwamo na kiongozi wa juu katika chama hicho Mohamed Badie.

Malalamiko yanayochunguzwa na ofisi ya mwendesha mashtaka ni pamoja na uchochezi na kuzorotesha uchumi wa Taifa hilo lililopitia mapinduzi mengine mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak.

Badie pamoja na viongozi wengine wa Muslim Brotherhood tayari wanakabiliwa na mashtaka mengine dhidi ya uchochezi ingawa hakuna yeyote kati yao ambaye amekwishakamatwa.

Wakati huo huo wafuasi wa Morsi wameendelea kuandamana kwa zaidi ya juma moja sasa wakipinga mapinduzi yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo, watu zaidi ya 90 wanakadiriwa kupoteza maisha katika machafuko yaliyoambatana na maaandamano hayo.

Marekani na Ujerumani tayari zimetoa wito kwa jeshi kumuachia huru Morsi, hata hivyo viongozi wa serikali ya mpito wanasema Morsi ambaye hajaonekana hadharani toka kupinduliwa kwake amehifadhiwa mahali salama.