TANZANIA

Miili ya wanajeshi saba wa Tanzania kukabidhiwa kwa ndugu kesho Jumatatu baada ya kuwasili Dar es Salaam jana Jumamosi

wanajeshi wa jJWTZ wakiwa wamebeba mwili wa mmoja wa wanajeshi waliouwawa huko Darfur
wanajeshi wa jJWTZ wakiwa wamebeba mwili wa mmoja wa wanajeshi waliouwawa huko Darfur

Miili ya wanajeshi saba wa jeshi la Umoja wa Afrika raia wa Tanzania ambao waliuawa kufuatia shambulio huko Darfur nchini Sudani imepokelewa jana jijini Dar es salaam nchini Tanzania tayari kwa taratibu za mazishi. 

Matangazo ya kibiashara

Miili hiyo imepokelewa kwenye uwanja wa anga la jeshi la wananchi jijini Dar es Salaam na kupokelewa kwa simanzi na wanajeshi wa JWTZ pamoja na ndugu jamaa na marafiki waliofika kwa wingi  uwanjani hapo.

Wakiwa na nyuso za maombolezo baadhi ya wafiwa wametoa wito kwa jumuiya za kimataifa na umoja wa Afrika kuwa makini kwa kuhakikisha usalama wa vijana na walinda amani wanaotumwa kulinda amani katika mataifa mbalimbali.

Msemaji wa JWTZ Meja Joseph Masanja amesema kuwa baada ya miili hiyo kuwasili taratibu mbalimbali za jeshi hilo zitafanyika na kisha miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu zao kwa taratibu za maziko.

Hapo awali Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Fatou Bensuda ametoa onyo kali kuhusu shambulizi la hivi karibuni lililowalenga waangalizi wa amani kutoka Umoja wa Mataifa na jeshi la umoja wa afrika huko Darfur Sudan UNAMID na kusema kuwa linaweza kuhesabika kama uhalifu wa kivita.

Katika taarifa yake akiwa Heague Fatou Bensuda amekumbusha pande zote zenye mgogoro kufahamu kuwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ina mamlaka jimboni Darfur.

Mnamo tarehe 13 mwezi Julai wanajeshi saba wa kulinda amani raia wa Tanzania waliuawa na wengine kumi na saba kujeruhiwa baada ya shambulizi kutekelezwa na kundi ambalo halijafahamika huko Darfur nchini Sudani.