SYRIA-URUSI

Naibu Waziri Mkuu wa Syria Jamil yupo nchini Urusi kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Lavrov juu ya mazungumzo ya Geneva

Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil yupo nchini Urusi kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Sergie Lavrov
Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil yupo nchini Urusi kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Sergie Lavrov

Serikali ya Urusi imeendelea kuwa kinara wa kuhakikisha umwagaji wa damu uliodumu kwa miezi ishirini na nane nchini Syria unamalizwa na hii leo unatarajiwa kukutana na Naibu Waziri Mkuu wa Serikali ya Damascus Qadri Jamil kuangalia mbinu za kukomesha machafuko yanayoendelea.

Matangazo ya kibiashara

Naibu Waziri Mkuu Jamil ameelekea huko Moscow nchi ambayo imekuwa upande wa Syria tangu kuanza kwa machafuko hayo kufanya mazungumzo na Viongozi wa Serikali kabla ya kufanyika kwa mazungumzo ya Geneva kati yao na Viongozi wa Upinzani yanayosimamiwa na Urusi pamoja na Marekani.

Mazungumzo haya ya Naibu Waziri Mkuu Jamil ni muendelezo wa harakati za kuhakikisha mkutano wa Geneva unafanyika kama ambavyo umepangwa na ikiwezekana utokeo na suluhu ya kudumu juu ya machafuko yanyoendelea nchini Syria.

Jamil anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Moscow Sergie Lavrov ambaye amekuwa sehemu ya maandalizi ya mazungumzo ya Geneva akishirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry.

Viongozi hao baada ya kufanya mazungumzo yao faraghani wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari kueleza kile walichoafikiana kabla ya kufanyika kwa mazungumzo hayo ya Geneva ambayo yamekuwa yakikosolewa pakubwa na Upinzani.

Mkutano huu unakuja huku taarifa zikionesha machafuko na mapigano yaliyoendelea siku ya jumapili nchini Syria yakisababisha vifo vya watu themanini na mbili kwa mujibu wa Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu.

Katika tukio la kwanza lililotokea Kaskazini Magharini mwa Damascus lilisababisha vifo vya raia kumi na wanane huku waasi ishirini na nane wakipoteza maisha baada ya kupambana na wanajeshi wa Serikali.

Jeshi linalomtii Rais Bashar Al Assad likipata usaidizi kutoka kwa Wanamgambo wa Hezbollah na Wanajeshi wa Iran wameendelea kutoa wakati mgumu kwa wapiganaji wa waasi kwenye maeneo wanayoyashikilia.

Wanajeshi wa Serikali wanatajwa kuendelea kusonga mbele huku wakijiapiza kuhakikisha wanarejesha kwenye himaya yao maeneo yaliyoangukia kwenye mikono ya wapinzani ambao wanaonekana kuanza kukosa nguvu waliyokuwa nayo awali.