SYRIA-URUSI

Urusi yaitaka Serikali ya Syria kufanyakazi pamoja na Upinzani kuyamaliza Makundi ya Kigaidi na yale yenye Msimamo Mkali

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil

Serikali ya Urusi imetoa wito mpya kwa Serikali ya Syria na Upinzani nchini humo kufanyakazi pamoja katika kuhakikisha wanawafurusha magaidi pamoja na makundi mengine yenye msimamo mkali yaliyokita mizizi katika ardhi yao. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov ndiye ametoa tamko la Serikali ua Moscow alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Damascus Qadri Jamil na kusema hiyo itakuwa njia mojawapo ya kumaliza mapigano yanyoendelea.

Matangazo ya kibiashara

Lavrov amekiri nchi yake kusikitisha na umwagaji wa damu ulioshuhudiwa kwa kipindi cha miezi ishirini na nane ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na uwepo wa makundi yenye msimamo mkali nchini Syria.

Waziri huyo mwenye dhamana ya masuala ya mambo ya kigeni ya Urusi ameweka bayana huu ni wakatimuafaka kwa Baraza la Taifa la Upinzani nchini Syria kushirikiana na Serikali ya Rais Bashar Al Assad katika kushughulikia mgogoro uliopo.

Lavrov amekutana na Jamil ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa maandalizi wa mazungumzo ya Geneva ambayo yamekuwa yakisimamiwa na mataifa ya Urusi na Marekani yakiwa na lengo la kuzileta mezani pande zinazohasimiana.

Naibu Waziri Mkuu wa Serikali ya Damascus Jamil amewaambia wanahabari baada ya kukamilisha mazungumzo yake na Lavrov ya kwamba wao wapo tayari kufanyakazi na Upinzani iwapo tu watafuata masharti.

Urusi imekuwa mshirika mkubwa wa Serikali ya Damascus na inafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha umwagaji wa damu uliogharimu maisha ya watu zaidi ya 100,000 unamalizwa nchini Syria.

Katika hatua nyingine mazungumzo hayo yamejadili hatua ya Moscow kuendelea kutoa msaada na mkopo zaidi kwa Damascus ili iweze kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi inayopitia kwa sasa.

Taarifa zinasema Moscow ipo tayari kutoa msaada kwa Damascus ikiwa ni pamoja na kuwapa zana zaidi za kivita kukabiliana na mapigano yanayofanywa na wapinzani wanaotaka kuingusha Serikali ya Rais Assad.