JAPAN

Waziri Mkuu wa Japan Abe ajiapiza kufanya mabadiliko ya kiuchumi sanjari ya kukabiliana na tatizo la ajira baada ya Chama Chake kushinda Uchaguzi

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ameahidi atafanya mabadiliko ya uchumi na kukabiliana na tatizo la ajira
Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ameahidi atafanya mabadiliko ya uchumi na kukabiliana na tatizo la ajira REUTERS/Yuya Shino

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amefanikiwa kukiongoza Chama Chake kushinda viti vingi kwenye uchaguzi wa wabunge uliofanyika jana nchini humo na sasa atakuwa na kibarua kikubwa cha kuhakikisha anashughulikia tatizo la ajira lililopo.

Matangazo ya kibiashara

Chama cha Liberal Democratic anachotoka Waziri Mkuu Abe kimeweza kuvuna zaidi ya nusu ya viti mia moja ishirini na moja vilivyokuwa vinawaniwa kwenye kinyang'anyiro hicho ambapo moja ya sera zao zilikuwa ni kukabiliana na ajira sanjari na kufanya mabadiliko ya uchumi.

Waziri Mkuu Abe baada ya kuona Chama chake kikiwa kimepata wabunge wengi aliwaambia wanahabari hatua hiyo itamsaidia kuweza kuunfa Baraza la Mawaziri thabiti ambalo litakuwa na kazi kubwa ya kuwatumikia wananchi wa taifa hilo.

Japan kwa sasa inapita kwenye wakati mgumu kiuchumi kitu ambacho kimechangia nchi hiyo kushika nafasi ya tatu duniani kama taifa lenye uchumi imara nyuma ya Marekani na China ambazo zimeendelea kutawala uchumi wa dunia kwa sasa.

Abe amesisitiza huu ni wakati mzuri kwa Chama chake kuhakikisha kinabuni ajira mpya ambazo zitasaidia kumaliza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi ambao wamekuwa wakiikosoa serikali hiyo ya Tokyo.

Vyama vya Kutetea Maslahi ya Wafanyakazi nchini Japan vimesema kauli hiyo ya Waziri Mkuu Abe ya kwamba serikali yake itatengeneza ajira zaidi imewashangaza na hawajui itatekelezwa vipi.

Kiongozi wa Chama Cha Wafanyakazi Vijana Jijini Tokyo Makoto Kawazoe amekuwa ni miongoni mwa wale walioachwa kwenye maswali yaliyokosa majibu kutokana na kauli hiyo ya Waziri Mkuu Abe.

Wachambuzi wa Masuala ya Kiuchumi nchini Japan wamekiri bado Serikali ya Waziri Mkuu Abe itakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha inafanya mabadiliko ya kiuchumi katika kipindi kifupi pamoja na kushughulikia tatizo la ukosefu wa ajira linalowakabili wananchi wengi.