BRAZIL

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis anatarajia kuhudhuria Kongamano la Vijana nchini Brazil

Bango la Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis likiwa limewekwa katika Mji wa Aparecida
Bango la Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis likiwa limewekwa katika Mji wa Aparecida REUTERS/Paulo Whitaker

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis anatarajiwa kuongoza mamia ya vijana waliopo nchini Brazil kwa lengo la kuhudhia Siku ya Vijana Duniani ambapo tayari maelfu yao wameshaanza kukusanyika katika Miji mbalimbali.

Matangazo ya kibiashara

Papa Francis anatarajiwa kutoa ujumbe mzito kwenye Siku hiyo ya Vijana Duniani ambao akiongozwa na kauli mbiu ya “Kanisa kwa Maskini” ili kuweza kuwahamasisha vijana kuendelea kuwa karibu na kanisa.

Mkutano huo mkubwa umepangwa kufanyika katika Mji wa Aparecida ambao maelfu ya vijana wanatarajiwa kuwa karibu na Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani anayefanya ziara yake ya kwanza tangu apatiwe wadhifa huko.

Watu wanakadiriwa kufikia 35,000 wanatarajiwa kujumuika pamoja katika Mji wa Aparecida kwa ajili ya shughuli hiyo ambapo pia vijana watapata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali yanayowakabili.

Ziara hiyo wa juma moja ya Papa Francis ilianza vibaya baada ya kupokelewa kwa maandamano yaliyogeuka na kuwa ghasia kitu kilicholazimisha Jeshi kutumia nguvu kuwasambaratisa maelfu ya wananchi waliojitokeza kupinga ziara yake.

Papa Francis anaelezwa ataongoza misaa maalum ambayo itawajumuisha watu 15,000 ambao watakuwa ndani ya Kanisa huku wengine 20,000 wakiwa nje ambapo duru za usalama zinasema askari na wanajeshi 5,000 watashika doria.

Serikali ya Brazil imeendelea kuhakikisha usalama unaimarika kipindi hiki cha ziara ya papa Francis wakihofia kuendelea kushuhudiwa kwa maandamano yenye lengo la kupinga ziara hiyo.

Wananchi wa Brazil wameendelea kufanya maandamano wakitaka Serikali ya Rais Dilma Rousseff kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha wanaboresha maisha ya wananchi wa Taifa hilo.

Maandamano hayo nusura yatatize Mashindano ya Kombe la Mabara yaliyoandaliwa mapema mwezi uliopita nchini Brazil na kushuhudia wananchi wakiandama kila uchao kushinikiza yasifanyike.