MISRI

Mkuu wa Majeshi nchini Misri Jenerali Al Sisi atoa wito kwa wananchi kufanya maandamano ya kitaifa siku ya Ijumaa

Mkuu wa Majeshi nchini Misri Jenerali Abdel Fattah Al Sisi akihutubia taifa kwa njia ya Televisheni
Mkuu wa Majeshi nchini Misri Jenerali Abdel Fattah Al Sisi akihutubia taifa kwa njia ya Televisheni

Mkuu wa Majeshi nchini Misri Jenerali Abdel Fattah Al Sisi ametoa wito wa kufanyika ya kitaifa ambayo yatampa mamlaka yeye ya kupambana na vitendo vya ugaidi pamoja na machafukoyanyoendelea kushuhudiwa kipindi hiki wafuasi wa Mohamed Morsi wakipinga kitisho hicho. Jenerali Al Sisi ametoa tamko hilo kupitia hotuba yake iliyorushwa kupitia Televisheni ya Taifa akiwahamasisha wananchi wa Misri kujitokeza kwa wingi kwenye maandamano ya kitaifa ambayo ametaka yafanyike siku ya Ijumaa ikiwa ni ishara ya kumpa fursa ya kukabiliana na vitendo vinavyokwenda kinyume cha sheria.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyo wa Kijeshi ambaye aliongoza mchakato wa kumuondoa madarakani Morsi tarehe 3 ya mwezi Julai amesema anahitaji uungwaji mkono kutoka kwa wananchi wa Misri ili aweze kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na vitendo vya kigaidi vilivyoanza kuchomoza.

Wito wa Jenerali Al Sisi unakuja kipindi hiki ambacho wafuasi wa Morsi wameendelea kufanya mashambulizi wakishinikiza kuachiwa kwa Kiongozi huyo wa Chama Cha Muslim Brotherhood ambaye yupo chini ya uangalizi wa Jeshi tangu aondolewe madarakani mapema mwezi huu.

Jenerali Al Sisi ameweka wazi nia yake ni kupambana na machafuko pamoja na vitendo vyote vya kigaidi vinavyofanyika nchini Misri ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mashambulizi yanayotekelezwa kwa kutumia mabomu.

Kiongozi huyo wa Kijeshi nchini Misri amesema kumekuwa na machafuko yanayoendelea kila uchao yanayoratibiwa na Makundi ya watu wenye silaha kitu ambacho kinachangia kuzorotesha hali ya usalama wa Taifa hilo.

Jenerali Al Sisi amekanusha vikali madai ya kwamba amemsaliti Mohamed Morsi aliyemteua kushika wadhifa huo na badala yake amesema Kiongozi yoyote anapaswa kuongozwa kwa misingi inayoridhiwa na wananchi na si kinyume na hapo.

Takwimu zinaonesha watu zaidi ya 200 wameshapoteza maisha nchini Misri tangu Morsi aondolewe madarakani na Jeshi ambapo wafuasi wa Chama chake cha Muslim Brotherhood wakajitokeza mitaani wakijiapiza kushinikiza arudishwe madarakani.

Viongozi wa Chama Cha Muslim Brotherhood amesema hawatatishwa na kalu ya Jenerali Al Sisi na badala yake wataendeleza maandamano yao hadi pale ambapo Kiongozi wao ataachiwa na kukabidhiwa madaraka aliyoporwa.

Chama Cha Muslim Brotherhood kimetoa wito kwa wafuasi wake kutorudi nyuma na badala yake kuongeza shinikizo na kushikilia msimamo wao hadi pale sauti zao zitasikika na Mohamed Morsi kukabidhiwa wadhifa wake alioupata kwa njia za kidemokrasia.