ZIMBABWE

Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Zimbabwe ZEC yatangaza kutoa vitambulisho kwa Waangalizi 20,000 wa Uchaguzi wa Urais

Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Zimbabwe ZEC Joyce Kazembe akizungumza na waandishi wa habari
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Zimbabwe ZEC Joyce Kazembe akizungumza na waandishi wa habari

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Zimbabwe ZEC imetangaza kutoa vitambulisho kwa waangalizi wapatao 20,000 ambao watakuwa mashuhuda wa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

ZEC imesema zoezi hilo la utoaji wa vitambulisho kwa waangalizi linakwenda sanjari na kutoa huduma kama hiyo kwa waandishi wa habari ambao watakuwepo nchini Zimbabwe kwa ajili ya kukusanya habari wakati wa uchaguzi na baadaye ya uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti wa ZEC Joyce Kazembe akizungumza na waandishi wa habari pamoja na waangalizi hao amesema hadi sasa wameshatoa vitambulisho 18,000 kwa waangalizi wa ndani na vitambulisho 1,500 kwa waangalizi kutoka nje.

Kazembe amesema zoezi hilo lingali linaendelea na litafungwa rasmi siku nne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo uamuzi ambao umetolewa kwa kuwa Tume Huru ya Uchaguzi ZEC inataka ijue kabisa idadi ya vitambulisho ilivyotoa.

Tume Huru ya Uchaguzi ZEC imesema waangalizi ambao wamepewa vitambulisho hivyo watakuwa na ruhusa ya kuangalia kile kitakachokuwa kinafanyika kwenye vituo 9,650 vya kupigia kura vitakavyokuwa kwenye kata 1,958 nchi nzima.

ZEC imesema pia kila Ubalozi ambao upo nchini Zimbabwe umepewa nafasi zisizozidi tano za waangalizi wake huku pia Mashirika yote yasiyo na Kiserikali yakipewa fursa ya kufanya uangalizi pamoja na makanisa kutoka majimbo kumi.

Makamu Mwenyekiti wa ZEC amethibitisha hadi kufika sasa wameshatoa vitambulisho 294 kwa waandishi wa habari wa ndani huku waandishi 28 kutoka nje nao wakipewa ruhusa hiyo ya kuripoti uchaguzi huo.

Tume Huru ya Uchaguzi imeendelea kusisitiza waangalizi kutoka nchini Marekani na mataifa wanachama ya Umoja wa Ulaya EU hawataruhusiwa kushiriki kwenye zoezi hilo kutokana na wao kuiwekea vikwazo Zimbabwe.

Waangalizi ambao wameshawasili nchini Zimbabwe ni kutoka Umoja wa Afrika AU, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC, COMESA pamoja na wengine ambao ni Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Uchaguzi Mkuu nchini Zimbabwe umepangwa kufanyika tarehe 31 mwezi Julai ambao kinyang'anyiro kikali kinatarajiwa kuwa kati ya Rais Robert Gabriel Mugabe anayetetea wadhifa wake dhidi ya Mpinzani wake Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai.