MISRI

Hofu yatanda nchini Misri kabla ya kufanyika kwa Maandamano ya Kitaifa yaliyoitishwa na Mkuu wa Majeshi Jenerali Al Sisi

Jeshi nchini Misri limeanza kuimarisha hali ya usalama kabla ya kufanyika kwa maandamano ya kitaifa yaliyoitishwa na Jeshi hilo kesho
Jeshi nchini Misri limeanza kuimarisha hali ya usalama kabla ya kufanyika kwa maandamano ya kitaifa yaliyoitishwa na Jeshi hilo kesho REUTERS/Asmaa Waguih

Hofu imeanza kutanda nchini Misri kabla ya kufanyika kwa maandamano makubwa yaliyoitishwa na Jeshi nchini humo lililowataka wananchi kujitokeza siku ya Ijumaa kufanya maandamano ya kitaifa ambayo yatatoa ruhusu kwa jeshi kukabiliana na vitendo vya kigaidi na kumaliza machafuko. Hali hiyo imeibuka nchini Misri kutokana na wafuasi wa Chama Cha Muslim Brotherhood ambao wanamuunga mkono Mohamed Morsi aliyeondolewa madarakani na Jeshi kusema wataendelea na maandamano yao na wala hawatishwi na tamko la jeshi lililoitisha maandamano ya kitaifa. Wafuasi wa Morsi na wale ambao wanaunga mkono uamuzi wa Jeshi wameanza kujiandaa kila upande kuhakikisha wanafanikisha maandamano yao ambayo huenda yakageuka kuwa ghasia na kuchangia machafuko zaidi katika nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi limesema litaimarisha hali ya usalama nchi nzima kuhakikisha maandamano hayo ya kitaifa yanafanyika kwa amani na utulivu bila ya kuingiliwa kwa namna yoyote na makundi ya kigaidi ambayo yamejiapiza kutatiza shughuli hizo muhimu kwa taifa hilo.

Wafuasi wa Chama Cha Muslim Brotherhood wamesema vitendo ambavyo wanavifanya wao si vya kigaidi kama ambavyo Jeshi limedai na ndiyo maana wataendelea na maandamano hayo kushinikiza kuachiwa kwa Morsi na kisha kurejeshwa madarakani.

Kiongozi mashuhuri wa Chama Cha Muslim Brotherhood Mohamed Badei ametoa wito kwa wananchi wa Misri kwa kutumia njia za amani kuhakikisha wanasimama kidete kupigania uhuru na kupambana na mapinduzi ya kumwaga damu.

Mkuu wa Majeshi nchini Misri Jenerali Abdel Fattah Al Sisi ndiye aliitisha maandamano hayo ya kitaifa akiamini kufanyika kwake kutoa ruhusu kwa jeshi kuhakikisha linamaliza kabisa vitendo vya machafuko na vile vya kigaidi.

Marekani yenyewe imekiri kuguswa na uamuzi wa Jenerali Al Sisi kuitisha maandamano hayo ya nchi nzima ambayo yakifanyika yatakuwa yametoa fursa kwa jeshi kuanza mchakato wa kupambana na ugaidi pamoja na machafuko yanayoendelea.

Wafuasi wa Chama Cha Muslim Brotherhood wameendelea kuandaa maandamano na kupambana na askari mara kadhaa tangu jeshi lilipomuondoa madarakani Mohamed Morsi tarehe 3 mwezi Julai huku wao wakishinikiza kuheshimiwa kwa demokrasia.